Matukio wanajamii kusingizia machafu kwa watoto wetu, yanatumaliza wenyewe

By Tuntule Swebe , Nipashe
Published at 08:52 AM Feb 28 2025
Watoto.
Picha:Mtandao
Watoto.

WAKATI mwingine kumekuwapo matabaka katika familia, kutokana na watu wengi kukosa elimu ya ukuaji watoto, wakisahau hatua za ukuaji watoto zinatofautiana.

Hiyo ina ushuhuda wa kuwapo fikra hasi zinazohusisha imani za kishirikina kwa watoto na wanajamii kwa upana.

Kuna wakati, nilishuhudia katika tovuti mojawapo ya chombo cha habari kimataifa, historia ya mkazi nchini anayeishi China, amekutana na changamoto, baada ya kupata mtoto wake wa pili aliyechelewa kuongea.

 Familia yake nyumbani ikaingiwa na shaka, hata pale alipofikisha umri wa miaka miwili, anaopaswa walau kupata uwezo wa kuongea, kama ilivyo kawaida kwa watoto wengine wa umri wake.

Mzazi huyo ana simulizi: ''Nilipokuwa nikimpeleka kliniki mjini Beijing, China nilimuuliza daktari kwanini huyu anachelewa kuongea?

Daktari alinijibu kwamba, hali hiyo ya kuchelewa kuongea mara nyingi hutokea kwa watoto raia wa kigeni.”

Tabibu huyo akasimulia, wapo wanaofundishwa lugha zaidi ya moja kwa wakati mmoja na inawachanganya.

Lakini, hoja hiyo kwa mama huyo hakuiafiki sana kwa  utetezi wake, “tafiti zinaeleza, kadri mtoto anavyozoeshwa kufahamu lugha nyingi, ndivyo anavyokuza akili na uwezo wake kufikiri.”

Mama huyo Mtanzania, ambaye amekuwa ughaibuni takribani  miaka 19, sasa yu mzoefu wa kuhudumu nyanja mbalimbali za kimataifa,

Ni hatua inayomwongezea ufahamu anaoutumia kuwasaidia wazazi wengine wenye watoto wenye usonji au hali kama hiyo.

Anaeleza kuwa mtoto wake katika umri wa miaka miwili na nusu, mwaka 2008, alirejea naye nyumbani Tanzania, akilengaa kumbatiza. 

Ndugu yake mmoja alimuuliza kuhusu hali ya mtoto huyo wa pili na kumshauri kwenda kwa madaktari bingwa wa mfumo wa ufahamu atakaporejea nchini China.

 Alifanya hivyo, huku jamii ikianza kumjadili vibaya, kuwapo baadhi walioamini kuwa alirogwa.

Hivyo ndivyo mama huyo alivyokumbana na imani za kishirikina, kwani baadhi ya watu waliamini mama kamroga mwanawe, hata kuleta utata kwa ndugu wengine.

Ndipo inapochokonoa hoja yangu, sisi umma kama waungwana, inatupasa kuwa na hofu kwa familia zetu kwa “wenye nacho wasiweze kuwatenga wasio nacho.”

Uhalisia ni kwamba wanahitaji msaada, hivyo watumike kama chachu ya kuwawezesha, wakiwapa mitaji, kuwawezesha kumudu mahitaji yao ya msingi.

Hata hivyo, kurejea ukweli kuna baadhi ya watu wanatenga ndugu zao kwa sababu ya magonjwa kama vile kifua kikuu.

Jambo hilo halijakaa sawa, kwani usahihi ni kwamba wanatakiwa kuishi na wagonjwa kisahihi, sio kuwatenga, wanatakiwa wakumbuke kila mmoja anaweza kukumbwa na ugonjwa, wakati wowote. 

Kwenye ngazi za ofisini na kwingineko kazini, nako kuna wanaotakiwa kuishi kwa umoja, wakipeana elimu ya ukuaji watoto, kamwe isiwe kutengana, kwa sababu ya vyeo au kipato au hata viburi na dharau kwa namna yoyote.

Ni jambo litasaidia makuzi ya watoto  na kuleta muunganikio kwenye shughuli zote za kazi, iwe katika majumba au vyumba vya kupanga.

Wapo baadhi ya wapangaji katika makazi hawajapata elimu ya makuzi ya watoto. Wamekuwa wakiamini ushirikina zaidi kwenye malezi na kuwa wao ni bora kuliko wengine. 

Hiyo ni kuanzia kuwashutumu wazazi na walezi wenye watoto wanaoumwa, kwa sababu tu watoto wao hawana shida zozote za kiafya. 

Wanachosahau ni kwamba, nadharia na ukweli kwamba ‘watu wote ni sawa.’ Hivyo, inakuwa muhimu kwa kuwa na tahadhari, ikiendana na kujifunza hatua za ukuaji binadamu, kwani ni zilezile isipokuwa hali ya kuchelewa.

Jambo la busara ni kwa waishi kwa umoja na kutojiwekea matabaka yanayoweza kuleta mtafaruku usio na maana, baina ya watu.

Kufanya hivyo kwenye ngazi za familia, kunasaidia kupata kizazi kilicho imara.

 Hata kwenye nyumba za kupanga, tunaweza kuwajenga watoto wetu  kuwapa mwamko wa kutojiwekea madaraja, dhana hiyo ikienda shuleni kuwasaidia kifikra washirikiane kwenye masomo. 

Watu wote kwa ujumla, inatupasa tusimame na kuyapinga matabaka kwenye jamii, tukipata wageni wanapozuru kwetu, wajifunze kupitia umoja wetu ambao ni nguvu na utengano ni dhaifu.