KATIKA gazeti hili toleo la jana, kumekuwa na habari za kupaa kwa bei za vyakula mbalimbali huku baadhi ya wataalamu wakitoa maoni yao kuhusu sababu za hali hiyo na nini kifanyike.
Habari hiyo ilibainisha kwamba wastani wa bei ya maharage katika jiji la Dar es Salaam ni Sh. 3,700 kwa kilo huku mchele ukiwa wastani wa Sh. 3,000 na kilo ya mahindi Sh. 1,100. Bei hiyo ni kwa vyakula vinavyotegemewa na wananchi kwa ajili ya mlo kila siku kwa hiyo ni vigumu kufikiwa na wale wa kipato cha chini.
Ongezeko hilo la bei ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo inaonesha kuwa hali hiyo ni tangu Februari, mwaka jana hadi Februari, mwaka huu.
Kwa mwenendo wa bei ulivyozoeleka nchini, ni vigumu kwa bei hiyo kushuka kwa kuwa mtindo wa wafanyabiashara umekuwa hivyo miaka nenda miaka rudi. Hali hiyo pia inawaumiza wananchi wengi wasio na uwezo wa kumudu gharama hizo kutokana na kipato chao.
Hali ya kupanda kwa bidhaa hizo muhimu kwa maisha ya kila siku ya wananchi ni kuwapo kwa upatikanaji usioridhisha kutoka kwa wakulima kwenda mijini kunakohanikizwa na uzalishaji mdogo kutokana na sababu mbalimbali.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Haji Semboja, anasema hali hiyo inatokana na watu wengi hasa nguvu kazi, kutoka vijijini kuhamia mijini ambako wanadhani kuna fursa, hivyo kusababisha uzalishaji kushuka tofauti na zamani.
Sababu nyingine aliyoitaja ni mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamechangia kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya chakula. Alisema ili kuinua uzalishaji, kunahitajika mikakati madhubuti kama vile teknolojia za kisasa, kilimo biashara kwa maana ya uwekezaji kwenye mashamba makubwa na umwagiliaji.
Ni dhahiri kwamba ushauri wa Prof. Semboja si mara ya kwanza kutolewa na wataalamu tangu serikali ya awamu ya kwanza kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika na baadaye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa la Tanzania. Hata mpango wa kwanza wa maendeleo, uliweka bayana kwamba kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa hadi likaja Azimio la Iringa la mwaka 1972 la Siasa ni Kilimo.
Katika serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais (mstaafu) Kikwete, iliibuka Sera ya Kilimo Kwanza ambayo pamoja na mambo mengine ilihimiza umuhimu wa kilimo cha kisasa kupitia mapinduzi ya sayansi na teknolojia huku matumizi ya zana za kisasa, kilimo biashara na umwagiliaji vikipewa kipaumbele.
Aidha, serikali ya sasa imeibuka na mpango ujulikanao kama ‘Be Better Tomorrow’ ambao unahimiza vijana kujikita katika kilimo. Sambamba na mpango huo, serikali imekuwa ikiongeza bajeti katika kilimo kila mwaka huku ikihimiza umwagiliaji, utafiti na uzalishaji wa mbegu bora na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Kwa ujumla, serikali imekuwa ikichukua hatua na kuweka mikakati mbalimbali katika kuhakikisha sekta ya kilimo inapiga hatua na kuhakikisha inachangia kwa kiwango kikubwa katika pato la taifa, maendeleo ya uchumi na usalama wa chakula kwa ujumla.
Pamoja na ukweli huo, kuna kikwazo mahali ambacho kinafanya kilimo cha Tanzania kisitoe tija inayotakiwa. Kwa mantiki hiyo, kuna umuhimu wa kuyafanyia kazi yale yote yanayotajwa kuwa yanachangia kutokea kwa hali hiyo na hatimaye kufanya nchi iendelee kushindwa kusonga mbele.
Mtaalamu mmoja wa uchumi kutoka Rwanda ambaye alisoma Tanzania kuanzia sekondari hadi shahada ya kwanza UDSM aliwahi kusema Tanzania ina wataalamu wazuri katika mipango lakini shida ni utekelezaji. Ni vyema utekelezaji wa mipango ukatiliwa mkazo pamoja na tathmini na ufuatiliaji wa yale yanayopangwa kwa ajili ya maendeleo ya taifa, kilimo kikiwamo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED