Kufunga kwa Wakristo, Waislamu kulete maana halisi katika maisha

Nipashe
Published at 10:54 AM Mar 05 2025
Kufunga kwa Wakristo, Waislamu kulete maana halisi katika maisha.
Picha:Mtandao
Kufunga kwa Wakristo, Waislamu kulete maana halisi katika maisha.

WAUMINI wa madhehebu ya Kikristo, leo wanaanza maadhinisho ya majira ya Kwaresma ikiwa ni kumbukumbu ya njia ya mateso aliyoiendea mwokozi wao Yesu Kristo, hadi kufikia hatua ya kukamatwa, kuteswa, kufa na kutundikwa msalabani yapata miaka 2,000 iliyopita.

Ni kipindi cha siku 40 ambacho  kinaanza leo ikiwa ni siku ya Jumatano ya Majivu wakianza na ibada hiyo ambayo hufanyika kila Jumatano hadi itakapofika Ijumaa Kuu, siku ambayo Yesu Kristo alisulubiwa msalabani hadi kufa. Baada ya hapo hufuatiwa na sikukuu ya Pasaka ikiwa ni kuadhimisha kufufuka kwa Yesu Kristo.

Wakati  Wakristo wanaanza Kwaresma leo, waumini wa Kiislamu leo wanaingia siku ya nne ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao huhitimishwa baada ya siku 30 kwa kuadhimisha kwa Sikukuu ya Iddi El Fitri.  

Matukio hayo kwa mwaka huu, baada ya miaka mingi, yamegongana na yanafanya waumini wa dini hizo kuingia katika mfungo. Waumini wote hao, kwa kawaida wanafunga kula na kunywa chakula kutwa hadi majira ya jioni watakapopata futari na baadaye chakula kisha kuendelea nakufunga siku inayofuata.

Wakati hayo yakitokea, yako mambo ya msingi ya kuyatafakari kuhusu kufunga huko na maisha ya kila siku ya muumini wa dini husika. Mambo hayo yanabebwa na dhima nzima ya kufunga, yaani saumu.  Neno saumu, yaani kufunga maana yeke ni  kujizuia kufanya jambo au kitu fulani kwa ajili ya ibada. Kwa maana halisi, mtu anafunga kula na kunywa katika kipindi  hicho ili kufanya sala na kumtafakari Mungu.

Maandiko matakatifu yanaonya kwamba kufunga si kutoa nafasi ya watu kugombana wala kushindana au kuonekana mbele za watu kwamba yuko kwenye mfungo wala kujitaabisha nafsi yake kwa kutokula wala kunywa. Maandiko hayo yanasema saumu ni kufungua vifungo vya uovu au kuacha kutenda mabaya na kuwa huru dhidi ya anasa na mambo yafananayo na hayo. 

Zaidi ya hapo ni Kutenda matendo ya huruma kwa maana ya kuwagawia wenye njaa chakula, kusaidia masikini, yatima na wajane. Sambamba na hayo kuwasaidia nguo wasio nazo na kuwatembelea wagonjwa na kuwaombea. Kwa kufanya hivyo, maandiko yanaainisha kuwa mtu wa namna hiyo atapata thawabu na nuru ya Mwenyezi Mungu itamwangazia.

Kwa maana hiyo, kufunga kunapaswa kuendandana na matendo ya huruma na kutafuta amani na suluhu baina ya mtu na jirani yake, ndugu kwa ndugu, kuacha chuki na kurejesha upendo pale ulipotoweka. Kwa maneno mengine, funga ya mtu ni kubadilisha tabia na mwendendo wake kwa kuyaacha matendo mabaya ya yanayomchukiza Mwenyezi Mungu. 

Ili funga isiwe bure, mtu anapaswa kuacha chuki na jirani yake, kinyongo na mpendwa wake, hasira, wivu na choyo. Zaidi ya hapo, mambo hayo hayapaswi kuwa ya msimu bali yambadilishe mtu mwenendo wake na kuyaishi siku zote za maisha yake. 

Kwa Kufunga kwa Wakristo, Waislamu kulete maana halisi katika maisha. hiyo, funga ya sasa ya Wakristo na Waislamu katika Kwaresma na Ramadhani ni fursa nzuri kwa mwanadamu katika kumrudia Mungu wake na kuyaishi matendo mema kama ilivyonenwa katika maandiko kwamba dini safi ni kutazama wagonjwa, kusaidia yatima, wajane na wenye mahitaji na zaidi kujilinda na dunia na kujiepusha kutenda dhambi. 

Kwa kuyaishi mambo hayo na mengine, ni dhahiri kwamba wanadamu wataishi kwa amani na upendo wakitawaliwa na hofu ya Mungu. Jambo la muhimu katika kipindi hiki kwa waumini wa dini zote  ni kumrudia  Mungu kwa kuacha mambo maovu na kutenda mema.