Kwa hili, TFF isitengeneze dhana mbaya kwa mashabiki wa soka

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:07 PM Mar 03 2025
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF).
Picha: Mtandao
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF).

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF), kupitia Bodi yake ya Ligi (TPLB), limeufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, kutumika kwa michezo ya ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

Taarifa ilitolewa baada ya mchezo kati ya Tabora United na Dodoma Jiji kumalizika wiki iliyopita, ni kuwa miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni za Leseni na Klabu.

"Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia uwanja huo kwa michezo ya nyumbani zitalazimika kutumia uwanja mwingine kama kanuni inavyoelekeza, mpaka uwanja huo utakapofunguliwa baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF," ndivyo ilivyoeleza taarifa hiyo.

Binafsi, sipingi kabisa kuwapo kwa viwanja visivyokidhi vigezo kwani vinasababisha kusiwe na ladha ya soka kwa mashabiki ambao wengi wanapenda kuona mpira mzuri.

Nimekuwa muumini na kupiga vita viwanja vya aina hiyo kwani vinasababisha mechi iwe na kubutuabutua, pia kutengeneza majeraha kwa wachezaji.

Hata hivyo, kuna maswali mengi ya kujiuliza juu ya hiki ambacho kimetokea. Si kwamba ndiyo sahihi, lakini kama binadamu mwenye kuumiza kichwa, utashi na uhuru wa kuwaza, kikubwa vitu vinafikirisha kwenye hili. Na haya ninayojiuliza, baadhi ndiyo yanaulizwa na mashabiki wengi mitaani.

Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi muda mrefu tu haonekani kama unakidhi vigezo, inawezekana ulitakiwa kufungiwa muda mrefu uliopita, kwa nini iwe sasa?

Pia, uwanja huo hautofautiani na ule wa CCM Kirumba ambao majuzi, ulichezwa mchezo wa Ligi Kuu kati ya Pamba Jiji na Yanga, huku Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao akisema umempunguzia dozi, mbona wenyewe haujafungiwa baada ya mchezo?

"Tatizo kubwa lilikuwa ni uwanja, haukuwa mzuri, ni mgumu sana kucheza hasa mipira ya chini, ilikuwa ikidunda wakati mwingine kupoteza uelekeo kitu ambacho ni hatari sana, inawezekana tungefunga idadi kubwa ya mabao kama uwanja ungekuwa mzuri.

"Nadhani mashabiki wa soka wameona kwenye televisheni leo mipira mingi ya juu na pasi ndefu, kwa sababu wachezaji walikuwa wanashindwa kutuliza chini, kukokota kuanzisha mashambulizi kuanzia nyuma," alilalamika kocha wa Yanga. Na alikuwa sahihi kwa kile alichokieleza kwa jinsi tulivyokuwa tukiona pasi za chini zilivyokuwa zikipigwa, halafu mpira unakwenda mbele unaanza kudunda na kwenda juu wenyewe.

Huu haujafungiwa, lakini Ali Hassan Mwinyi umefungiwa, kitu ambacho kinafikirisha.

Kwa nini umefungiwa siku chache kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga, ambapo tarehe inaonesha kuwa ulitarajiwa kupigwa Aprili Mosi? Ikumbukwe kuwa msimu uliopita mechi ya Tabora United dhidi ya Yanga haikuchezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, badala yake ulipigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Desemba 23, 2023, Yanga ikishinda bao 1-0 lililofungwa na Stephane Aziz Ki. Ni kama kuna kujirudia hivi kwa kitu kama hicho kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Tayari, uongozi wa Tabora United umeshatangaza kuwa mechi zake za Ligi Kuu na Kombe la FA zitachezwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma. Ina maana kama kipindi chote hiki, kutakuwa na ucheleweshwaji wa maboresho basi mechi itapigwa Jamhuri kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Kwa nini Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi huwa mbovu zinapokaribia mechi dhidi ya Yanga tu kwa msimu wa pili mfululizo? Sisemi kama ndiyo utachezwa huko, kwani bado muda upo wa uwanja kurekebishwa na mechi ikarudishwa mjini Tabora na mashabiki wake kufurahia kuiona timu yao nyumbani dhidi ya Yanga kwa mara ya kwanza.

Nia hapa ni kujenga, kwa wakati huu ambapo maneno yamekuwa mengi juu ya udhaifu wa waamuzi, mdhamini aliyejikita kwenye klabu moja, kudhamini timu nyingine nyingi za Ligi Kuu, wachezaji kubeti, rushwa, kupangiana vikosi dhaifu, wenye mamlaka ya soka wanatakiwa kuwa waangalifu na vitu kama hivi ili wasiwe wanazidi kuwapa watu la kusema mitaani.