HITAJI la uwepo wa katiba mpya ni moja ya hoja ambazo zinajadiliwa mara kwa mara na wadau mbalimbali wakiwamo wa siasa ambao matamanio yao ni kuona mchakato wa kuipata unaharakishwa.
Mjadala huo ni miongoni mwa mambo yanayojadiliwa na wadau mbalimbali wakiwamo wanasiasa, ambao wanatamani nchi kuwa na katiba inayoendana na mazingira ya sasa au ya karne ya 21.
Mwaka jana mjadala huo ulipata msukumo mpya baada ya viongozi wa asasi za kiraia na wanaharakati kuungana na wanasiasa na kupaza sauti kwa hoja mbalimbali za kutaka kumalizika kwa mchakato wake.
Lakini pamoja na harakati hizo, ni vyema mchakato huo usitekwe na wanasiasa wakaweka mambo yenye maslahi ya vyama vyao, badala yake watambue kuwa katiba ni ya Watanzania wote.
Wanasiasa wapige debe ili ipatikane, lakini wasiwe na nguvu ya kuingiza mambo yenye maslahi ya vyama vyao, kwa sababu katiba ni kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi na watu wak, si kikundi fulani.
Maana yangu ni kwamba, wanapojadili kuwapo kwa katiba mpya, wajikite katika kunufaisha taifa na watu wake. Lakini pia ni vyema wananchi wakaelimishwa kuhusu umuhimu wa katiba ya nchi.
Yaliyotokea kwenye Bunge Maalum la Katiba wakati huo, ilionekana kuwa baadhi ya wajumbe waliegemea kwenye itikadi za vyama vyao walipokuwa wakijadili rasimu ya Katiba Mpya.
Kabla ya bunge hilo kumalizika, ilitokea sintofahamu iliyosababisha baadhi ya wajumbe wake kutoka vyama vya upinzani kulisusia wakidai kuwa limeegemea kwenye matakwa ya vyama si ya wananchi.
Wajumbe kutoka vyama vya upinzani waliosusa bunge hilo, waliungana na kuanzisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambao ulikuwa na nguvu kubwa, ingawa kwa sasa ni kama haupo tena.
Yaliyotokea kwenye Bunge Maalum la Katiba wakati huo, ilionekana kuwa baadhi ya wajumbe waliegemea kwenye itikadi za vyama vyao walipokuwa wakijadili rasimu ya Katiba Mpya.
Iwapo mazingira ya aina hiyo yataendelea kuwapo, ni wazi katiba inayotafutwa inaweza kuwa ya wanasiasa na sio ya wananchi. Hivyo, suala kushirikisha wananchi kwa kuwapa elimu ili wajue umuhimu wa katiba na manufaa yake kwao ni jambo ambalo halikwepeki.
Mchakato wa katiba mpya ulikwama mwaka 2014 baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba, ikaandaliwa Katiba Inayopendekezwa ambayo hadi leo inasubiri kupigiwa kura ya maoni.
Iwapo kutakuwa na haja ya kuwa na Bunge Maalum la Katiba, basi vyema washirikishwe wajumbe ambao hawana mrengo wa chama chochote ili ipatikane katiba yenye maslahi ya taifa.
Hilo likifanyika, ni wazi kutakuwa na katiba ambayo wananchi wenyewe wanaitaka na sio ya wanasiasa ambayo inazingatia maslahi ya vyama vyao badala ya umma na kusababisha msuguano.
Sio kwamba wanasiasa hawana umuhimu kwenye mchakato wa katiba mpya, bali ninamaanisha kwamba wasiwe na nguvu kubwa kuliko wadau wengine wasio na vyama, kwani wanaweza kurudisha yaliyotokea 2014.
Jambo la msingi ni kujadili jinsi ya kupata katiba mpya inayoendana na mazingira ya sasa kwa maslahi mapana ya nchi. Katika mazingira kama hayo, maslahi ya vyama yanawekwa pembeni.
Mchakato wa katiba mpya ulianza mwaka 2011 wakati wa serikali ya awamu ya nne, lakini baada ya kukwama, CCM imekuwa ikilaumiwa kuwa iliouvuruga na kusababisha ukwame.
Lawama za aina hiyo zinapaswa kufanyiwa kazi kama zina ukweli ndani yake lengo likiwa ni kuhakikisha hazijirudii hasa kwa kutambua kagtiba si ya wanasiasa bali ni ya Watanzania wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED