Marekani kujiondoa WHO ni janga kwetu, tuchukue hatua

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 11:39 AM Jan 30 2025
Rais wa Marekani, Donald Trump.
Picha: Mtandao
Rais wa Marekani, Donald Trump.

RAIS wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuondoa nchi yake katika uanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hatua ambayo huenda ikaathiri miradi mbalimbali ikiwamo ya afya, inayosimamiwa na shirika hilo katika nchi za Afrika.

Iwapo hatua ya kiongozi huyo itatekelezwa na kusitisha misaada kwa mashirika ya afya duniani, huenda kukawa na changamoto ya kupatikana kwa dawa za kufubaza makali ya UKIMWI ARV.

 Wakati kukiwa na utata huo, nadhani ni vyema Wizara ya Afya ikaanza kutafuta njia mbadala ya kupata dawa hizo, au kuwaambia wananchi wake jinsi ambavyo inajiandaa kuchukua hatua.

 Ikumbukwe kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofaidika na huduma hiyo ya dawa za ARV, hivyo ingekuwa ni vyema iwapo tathmini ya athari itafanyika na kuwa na njia ya kunusuru waathirika.

 Sio vibaya kuelekeza nguvu nyingi katika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo wakati nchi ikijipanga kutafuta nyingine ya kuhakikisha watu wake wanaotumia ARV wanaendelea kuishi.

 Kwa kawaida dawa hizo zimekuwa zikitolewa bure, hasa Marekani ambayo ni mfadhili, ikiwamo ya afya inapotangaza kujiondoa uanachama wa WHO, ni wazi dawa hizo huenda zisipatikane bure.

 Hali ikiwa hivyo, ni wazi wale ambao wanatumia ARV wanaweza kuumia zaidi kwa kukosa dozi na kuhatarisha maisha yao. Ndio maana ninashauri Wizara ya Afya ije na njia mbadala.

 Uhai wa watu hao unategemea dawa hizo ambazo hutolewa bure, lakini unapojitokeza utata huo, ni wazi sasa ni kuwapo kwa bejeti ya kununulia ARV ambazo inawezekana zikaanza kuuzwa.

 Tukifikia hapo, inawezekana wengine wakashindwa kumudu gharama na kujikuta wakipoteza maisha, kwa sababu ya kukosa dawa. Hivyo, suala la kujipanga upya kama nchi ni la muhimu ili kuokoa maisha ya wananchi.

 Utafiti wa Hali ya UKIMWI (Tanzania HIV Impact Survey - THIS 2022/23), unaonyesha kuwa kiwango cha Watu Wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI (WAVIU) Na Wanatumia Dawa za Kufubaza VVU (ARV) ni asilimia 97.9 kulinganisha na asilimia 93.6 mwaka 2016/17. 

Kwa utafiti huo ni wazi kwamba kiwango cha watu wanaotumia dawa na wamefubaza VVU kimeongezeka. Sasa kundi hilo kubwa linapokosa dawa hizo, linaweza kujikuta katika mazingira magumu.

Hivyo, kwa kuwa Rais huyo ametia saini ya amri ya kuanza mchakato wa kuiondoa nchi yake kuwa mwanachama wa Shirika la Afya Duniani, viongozi wetu hawana budi kuanza mchakato wa jinsi ya kutunusuru.

Uamuzi wake ni mzito wenye athari katika sekta mbalimbali, lakini hii ya afya ninaiona ni nzito zaidi, kwani bila imara mtu hawezi kufanya kazi ya kuzalisha mali iwe mijini au vijijini.

Kimsingi, uamuzi wa Rais huyo wa taifa kubwa, si kwamba unaweza kuathiri utendakazi wa WHO, bali hata huduma za shirika hilo katika nchi mbalimbali duniani ikiwamo Tanzania.

Wapo wanaosema kuwa kidonge kimoja cha ARV kinauzwa kwa gharama Sh. 300,000 hadi 400,000, lakini kwa kuwa Marekani alikuwa mwanachama, alihakikisha vidonge hivyo vinapatikana bure. 

Iwapo kweli bei yake ndio hiyo, sijui kama vitaendelea kupatikana bure. Huenda kujiondoa huko kunaweza kuchangia kupanda kwa bei ya dawa na kusababisha athari kubwa zaidi.

Inaelezwa kuwa mchango wa Marekani WHO ulikuwa ni asilimia 60 huku mataifa wengine yakichangia asilimia 40, kwa hali hiyo ni kwamba Wamarekani walikuwa na mchango mkubwa.

Ni wakati sasa kuweka mipango ya kujinusuru na janga linaloweza kujitokeza baada ya nchi hiyo kutangaza kujiondoa uanachama wa WHO ili kunusuru asilimia 97.9 ya watu wanaotumia.