Benki ya Azania yakabidhi pikipiki kwa kikundi cha Tujiendeleze Butiama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:12 PM Apr 15 2025
Meneja wa Benki ya Azania Roda Baluhya akimkabidhi mwanachama wa kikundi cha Tujiendeleze Jacline Ringo ufunguo wa pikipiki. Benki ya Azania imetoa pikipiki 10 kwa kikundi hicho lengo likiwa kuwasaidia waweze kujikwamua kiuchumi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja wa Benki ya Azania Roda Baluhya akimkabidhi mwanachama wa kikundi cha Tujiendeleze Jacline Ringo ufunguo wa pikipiki. Benki ya Azania imetoa pikipiki 10 kwa kikundi hicho lengo likiwa kuwasaidia waweze kujikwamua kiuchumi.

Benki ya Azania imekabidhi mkopo wa pikipiki 10 zenye thamani ya Shilingi milioni 30 kwa Kikundi cha Tujiendeleze kilichopo wilayani Butiama, mkoani Mara, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya vikundi.

Kikundi hicho chenye wanachama 31 – wengi wao wakiwa wanawake – kinajishughulisha na shughuli za kilimo, uchimbaji madini, na biashara ndogondogo. Kupitia mkopo huo, wanachama hao wanatarajiwa kutumia pikipiki kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo yao, kutoa huduma za bodaboda na kuongeza mapato ya kikundi kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya pikipiki hizo, Meneja wa Benki ya Azania tawi la Geita, Rhoda Baluhya, alisema benki hiyo inaendelea kutoa mikopo kwa watu binafsi na vikundi vilivyosajiliwa ili kuwawezesha Watanzania kuinuka kiuchumi.

"Tunatoa elimu ya fedha, namna ya kuweka akiba na kutumia mikopo kwa ufanisi. Pia tunawahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo," alisema Baluhya.

Kwa upande wake, mlezi wa kikundi hicho, Jacline Ringo, alisema mkopo huo ni sehemu ya mkakati wa kukuza mtaji wa kikundi, ili kufanikisha malengo yao ya kuanzisha viwanda vidogo vya uzalishaji wa sabuni na batiki.

1

"Lengo letu ni kutoka hatua moja kwenda nyingine kiuchumi. Pikipiki hizi zitatusaidia kupata mapato ya kuendesha shughuli zetu za kila siku na kukuza mtaji," alisema Ringo.

Naye mmoja wa wanachama wa kikundi hicho, George Nyamkura, alisema kabla ya kupokea pikipiki walikuwa wakitumia baiskeli au kubeba mizigo kwa kichwa, hali iliyokuwa ikichelewesha shughuli zao za kila siku.

"Hii ni hatua kubwa kwetu. Pikipiki zitasaidia kusafirisha mizigo ya uchimbaji na kilimo kwa urahisi, na pia tutaweza kutoa huduma za bodaboda kuongeza kipato," alieleza Nyamkura.

Benki ya Azania imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na vikundi mbalimbali nchini kuhakikisha vinapata mitaji na elimu ya kifedha, kwa lengo la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla.

2