Bosi TASAC asihi jamii kulinda mazingira ya Bahari

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:16 PM Sep 25 2025
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwaka wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwaka wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum.

Wakati, jamii ya kimataifa ya masuala ya bahari inaadhimisha Siku ya Usafiri Majini Duniani leo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwaka wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum ameiasa jamii kulinda mazingira ya bahari na kutumia fursa ya kipekee ya kutafakari, kutambua na kuthamini mchango muhimu wa sekta ya bahari katika kuunganisha dunia na kukuza biashara ya kimataifa kwa njia ya bahari.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari aliyoitoa, Bw. Salum amesema kuwa kaulimbiu ya mwaka huu.

“Bahari Yetu, Wajibu Wetu, Fursa Yetu” inatukumbusha umuhimu wa bahari na nafasi yake katika kuhifadhi na kusaidia uhai na bioanuwai ya viumbe wa majini, sambamba na kutoa mamilioni ya ajira duniani hasa katika usafirishaji, utalii, uvuvi, madini, mafuta na gesi, pamoja na ufugaji wa samaki.

Amesema kuwa Tanzania kama taifa lililo na bahari, imebarikiwa kuwa na rasilimali hii muhimu ya asili na hivyo wanajamii wana wajibu wa kuilinda. 

“Tangu enzi za kale, bahari imekuwa chanzo kikuu cha chakula na njia ya kusafirishia bidhaa, hasa kwa biashara ya kimataifa. Bahari inahusika kwa zaidi ya asilimia 60 ya uzalishaji wa hewaa ya oksijeni duniani na pia inachukua jukumu la msingi la kunyonya na kuhifadhi hewa ya ukaa. Pamoja na kuwa chanzo cha uhai, bahari pia ni makazi ya bioanuwai ya majini na mifumo ikolojia isiyo na kifani kwa akili ya binadamu,” amesema.

Ameongeza kuwa katika miongo ya hivi karibuni, shughuli za binadamu zimeathiri kwa kiwango kikubwa uwezo wa bahari kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Uchafuzi wa plastiki, kemikali kutokana na kilimo na viwanda, kumwagika kwa mafuta, uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa hewa na uchimbaji wa madini baharini vimeleta athari kubwa kwa bahari na bioanuwai ya majini.

“Hivyo, tuna wajibu wa kulinda bahari zetu unahitaji hatua za pamoja kutoka kwa watu binafsi, jamii na Serikali katika kushughulikia visababishi vikuu vya uchafuzi wa bahari. Uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa (CO₂) unasababisha asidi baharini, hali inayopelekea kuathiri viumbe vya majini. Hali hii uchangia ongezeko la joto duniani ambalo husababisha kupanda kwa viwango vya maji ya bahari na kutishia maisha ya jamii nyingi za visiwa vidogo. Hivyo basi, hii ni fursa kubwa kwa nchi kuchukua hatua za kuhakikisha ulinzi wa uhai wa viumbe vya majini kwa kuunga mkono usafirishaji endelevu, kupunguza uchafuzi wa plastiki na kuhimiza mabadiliko ya sera ili kuhakikisha tunailinda bahari yetu kwa vizazi vijavyo,” ameongeza. 

Amehitimisha kuwa tunapotafakari siku hii, ni wakati wa jamii na ni  fursa  ya kuhamasisha hatua stahiki kwa ajili ya ulinzi wa bahari kwa vizazi vijavyo na ustahimilivu wa sayari yetu, huku tukiendelea kutumia fursa za uchumi wa buluu.