CCM yaahidi meli mpya, kupeleka mazao Comoro

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 03:05 PM Oct 02 2025
Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ameahidi kujengwa kwa meli mpya itakayosafirisha mazao kutoka mkoani Mtwara kwenda Comoro, lengo likiwa ni kuwa na soko la uhakika la mazao na bei nzuri.

Pia, amesema ndani ya miaka mitano ijayo kutafanyika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara, ili uwe wa kimataifa kwa kuboresha majengo ya abiria, mnara wa kuongozea ndege na eneo la zimamoto.

Ametoa ahadi hizo leo Oktoba 02 eneo la Nanguruwe Mtwara vijijini wakati akihutubia wananchi wa eneo hilo, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

"Tunajua wakazi wa Mtwara ni wakulima wazuri wa korosho na mazao mengine lakini mnakabiliwa na tatizo la soko. Hivyo katika miaka mitano ijayo tutajenga meli mpya ya mzigo itakayokuwa ikibeba mazao ya wakazi wa Mtwara kwenda kuuza Comoro. Meli hiyo itakuwa inabeba mazao ya wakulima, lengo ni kuwa na soko la uhakika na bei nzuri," amesema Balozi Dk. Nchimbi.

Kwenye sekta ya kilimo, Balozi Dk. Nchimbi amesema serikali itakayoundwa na CCM miaka mitano ijayo itaongeza na kusimamia upatikanaji wa ruzuku ya mbolea na mbegu, kwa kuhakikisha wakulima mkoani Mtwara wanapata kwa wakati.