Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali itaendeleza jitihada za kuwawezesha wavuvi, wachuuzi na wajasiriamali ili kuongeza kipato chao na kukuza uchumi wa wananchi.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na wavuvi, wachuuzi wa samaki na wajasiriamali katika diko na soko la samaki la Malindi, ikiwa ni sehemu ya kampeni zake zinazoendelea kwa kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi.
Amesema serikali itaweka utaratibu mzuri wa usimamizi wa masoko ili kumaliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao katika maeneo yao ya kazi. Aidha, aliwahakikishia wananchi upatikanaji wa mikopo kwa wale ambao bado hawajapata katika awamu ya kwanza ya utoaji wa mikopo, na kuahidi ongezeko maradufu la fedha kutoka shilingi bilioni 96 zilizotolewa awali.
Dk. Mwinyi amebainisha kuwa serikali itaendelea kujenga madiko na masoko ya samaki pamoja na maeneo bora kwa wajasiriamali Unguja na Pemba. Pia, itawekeza katika vifaa vya kisasa vya uvuvi, ikiwemo boti na vitendea kazi vya kisasa, ili wavuvi waweze kuvua katika bahari kuu na kuongeza tija.
Akihitimisha Dk. Mwinyi amewaomba wavuvi, wachuuzi na wajasiriamali kumchagua tena katika uchaguzi ujao, akisisitiza kuwa utekelezaji wa ahadi hizo utaleta maendeleo zaidi kwa Zanzibar na wananchi wake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED