Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeshinda kwa mara ya pili tuzo ya Uhusiano Mwema na Vyombo vya habari nchini, kwa mwaka 2024.
Tuzo hiyo imetolewa na Chama cha Maofisa Uhusiano Tanzania (PRST) ambapo taasisi mbalimbali zilikuwamo kwenye mchuano wa tuzo hiyo.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo amesema ushindi huo kwa mara ya pili mfululizo ni kielelezo cha utawala bora, uwazi, uwajibikaji, na miongozo inayotolewa na Bodi na Menejimenti ya EWURA, chini ya mwemyekiti wake Prof. Mark Mwandosya na Mkurugenzi wake Mkuu, Dk. James Mwainyekule.
Amesema tuzo hiyo imeipa heshima EWURA na ari ya kuendelea kudumisha uhusiano wake thabiti na vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari nchini.
Wakati huo huo, Janeth Mesomampya, ambaye ni Ofisa Uhusiano wa EWURA amepokea tuzo ya Ofisa Uhusiano bora kwa mwaka 2024, akiwa mmoja wa washindi watano katika tuzo hizo.
Rais wa PRST, Assah Mwambene, amesema utoaji wa tuzo hizo ni chachu kwa wataalam walioko kwenye kada hiyo kufanya kazi zao kwa ubora zaidi ili kuimarisha huduma katika maeneo yao ya utendaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED