Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga, ameitaka Serikali kuharakisha ulipaji wa fidia ya Shilingi bilioni nne kwa wakazi wa Iboya ili kupisha ujenzi wa cheki point utakaochangia kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Tunduma.
Akizungumza leo bungeni jijini Dodoma wakati wa kuchangia hoja, Hasunga amesema wananchi hao wamesubiri fidia yao kwa muda mrefu, na akashauri kuwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, afanye mazungumzo na Wizara ya Fedha kuhakikisha fedha hizo zinapatikana.
"Cheki point hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji na kuinua uchumi wa taifa," amesema Hasunga.
Aidha, mbunge huyo alikumbusha ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapa fursa ya ukandarasi katika miradi ya barabara kupitia TANROADS. Alitaka ahadi hiyo kutekelezwa kwa vitendo kwa kuwapa wanawake wakandarasi kilomita tano kila mmoja, kama ilivyokusudiwa.
“Barabara iliyopendekezwa ni njia panda ya Iyula – Idiwili hadi Ngimbili yenye urefu wa kilomita 20. Tayari iko kwenye bajeti ya mwaka huu, lakini mchakato wa manunuzi haujakamilika. Wanawake tuliowahamasisha kuhama ili kupisha ujenzi wanasubiri kwa matumaini. Naomba mchakato huo ukamilishwe haraka ili waingie kazini,” amesema Hasunga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED