Korosho tani 370,000 zasafirishwa, ufanisi waongezeka kwa 46%

By Baraka Jamali , Nipashe
Published at 01:15 PM Oct 01 2025
Korosho
Picha: Mtandao
Korosho

BANDARI ya Mtwara imeendelea kung’ara kama kitovu cha usafirishaji mazao ya biashara nchini, baada ya kufanikisha usafirishaji tani 370,896 za korosho nje ya nchi kwa msimu wa 2024/2025.

Hatua hiyo inawakilisha ongezeko la asilimia 46.2 kutoka tani 253,616.94 zilizosafirishwa msimu uliopita.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, katika kikao cha wadau wa bandari kilichofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu – Mtwara, chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), mafanikio hayo yamevuka lengo la awali la tani 200,000 lililowekwa na mamlaka hiyo, na hata kupita makisio ya tani 300,000 yaliyotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania.

"Hadi kufikia Machi 31, 2025, tumefanikisha usafirishaji tani 370,896 za korosho nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 46 kulinganisha na msimu uliopita, na linaonesha kuwa tupo kwenye mwelekeo sahihi," alisema Nyathi.

Akifafanua zaidi, meneja huyo alibainisha kuwa mafanikio hayo yamepatikana licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ukiwamo uhaba wa mitambo, ufinyu wa maeneo ya kuhifadhi shehena na mlundikano wa meli wakati wa kilele cha msimu.

"Tulichukua hatua za haraka ikiwamo kuongeza mitambo mipya, kutenga maeneo ya akiba kuhifadhi korosho, pamoja na kuzipa kipaumbele meli zilizokuwa tayari kupakia," aliongeza.

Kwa msimu ujao wa 2025/26, Bandari ya Mtwara inalenga kuhudumia zaidi ya tani 367,000 za korosho, huku makisio ya kitaifa yakitarajiwa kufikia tani 700,000.

Mikakati ya kuongeza ufanisi inajumuisha kutoa mafunzo endelevu kwa wafanyakazi na wateja, kushirikiana na sekta binafsi katika ufungashaji, matumizi ya mtambo mpya wa SSG, mikataba ya kukodisha mitambo ya kisasa, pamoja na kupunguza gharama za huduma kwa wateja.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, aliwataka wadau wote wa sekta ya usafirishaji na biashara ya korosho kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha korosho zote kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zinasafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara.

"Nitoe rai kwa wadau wote kuendelea kutumia Bandari ya Mtwara kama lango kuu la biashara ya korosho. Hatua hii si tu inaleta ajira kwa wananchi, bali pia inaongeza mapato ya serikali na kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla," alisema Kanali Sawala.

Bandari ya Mtwara imeendelea kuwa mkombozi wa wakulima na wafanyabiashara wa korosho, kwa kuwawezesha kupata huduma za haraka, uhakika wa soko na kupunguza gharama za usafirishaji bidhaa hiyo muhimu ya kimkakati.

Mkutano huo wa wadau uliwaleta pamoja wakulima, wasafirishaji, viongozi wa serikali na mashirika binafsi yanayohusika katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho.