Manispaa ya Kibaha yasaini mkataba bilioni 19 kuboresha soko

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:15 PM Sep 25 2025
Manispaa ya Kibaha yasaini mkataba bilioni 19 kuboresha soko
Picha:Mpigapicha Wetu
Manispaa ya Kibaha yasaini mkataba bilioni 19 kuboresha soko

Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani imesaini mkataba na Mkandarasi DIMETOCIASA REAL HOPE LTD kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Mnarani na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, mradi wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 19.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi ya TACTIC, inayofadhiliwa na Serikali Kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia wenye thamani ya dola za Marekani milioni 410, ambao unatekelezwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika miji 45 nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mradi huo unalenga kuwapatia wananchi huduma bora na kuwahakikishia upatikanaji wa bidhaa katika mazingira salama.

Kunenge amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuzingatia muda uliopangwa ili wafanyabiashara waweze kurejea haraka katika shughuli zao, huku akiwataka wananchi kushiriki katika ulinzi wa vifaa vya ujenzi ili kuepusha hasara na ucheleweshaji wa utekelezaji.

Aidha, Kunenge amebainisha kuwa mradi huo ni nyenzo muhimu ya kuongeza kipato kwa wakazi wa Manispaa ya Kibaha na kutoa fursa za ajira.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, amesema ofisi yake itaimarisha usimamizi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.

Naye Mratibu Msaidizi wa Miradi ya Benki ya Dunia kutoka TAMISEMI, Mhandisi Emanuel Manyanga, amesema mradi huo unatarajiwa kuanza Oktoba mosi na kukamilika ndani ya miezi 15. Alifafanua kuwa mbali na uboreshaji wa soko na barabara, mradi utahusisha pia ujenzi wa bustani ya mapumziko.

Akizungumzia programu ya TACTIC, Mhandisi Manyanga amesema lengo lake si tu kuboresha miundombinu ya miji, bali pia kujenga uwezo wa Halmashauri katika usimamizi wa maendeleo ya miji na ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Mnarani, Mohamed Mnembwe, ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo, akisema utaboresha mazingira ya wafanyabiashara na kuchochea shughuli za kiuchumi.