Mgombea urais CHAUMMA aahidi kupiga 'stop' mikopo “Kausha Damu”

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:30 PM Sep 26 2025
Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu.

Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, amesema iwapo atachaguliwa kuingia madarakani atapiga marufuku kampuni zote zinazowaingiza wananchi kwenye mikopo ya kinyonyaji maarufu kama kausha damu.

Mwalimu amesema haiwezekani taifa kuendelea kuendesha uchumi wake kupitia mfumo wa mikopo hiyo, ambayo badala ya kusaidia wananchi imekuwa ikiwadidimiza zaidi kwenye umasikini.

"Kuacha nchi hii iendeshwe kwa uchumi wa kausha damu ni kumkufuru Mungu, na hatuwezi kuacha hali hii iendelee. Nikipewa nchi, napiga marufuku kampuni zote zinazoleta kausha damu kwa wananchi," amesema Mwalimu.

Ameeleza kuwa chanzo kikuu cha wananchi wengi kukimbilia mikopo ya aina hiyo ni umasikini unaochochewa na kukosekana kwa sera thabiti za kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

Kwa mujibu wa Mwalimu, serikali ya CHAUMMA itakayoundwa chini ya uongozi wake, itajielekeza kwenye kuandaa sera za maendeleo ya kiuchumi zinazolenga kuinua kipato cha wananchi, badala ya kuwaachia wakandamizaji wachache kunufaika kupitia mateso ya wananchi walio wengi.