Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa kutumia kilimo cha viungo (Spice ) kama njia ya kuwakomboa wananchi wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla kutoka kwenye umasikini wa muda mrefu.
Akizungumza katika mara baada ya kuwatembelea wakulima hao Shehia ya Mtambwe Daya, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Othman alisema ardhi ya Pemba ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao yenye thamani kubwa duniani kama vile vanila, karafuu na pilipili hoho, lakini viongozi waliopo madarakani wameshindwa kutumia fursa hiyo kwa maendeleo ya watu.
Mgombea huyo wa ACT Wazalendo alisema changamoto hizo zinatokana na mifumo mibovu ya serikali iliyopo, ambayo haijali wakulima wadogo wala haikuweka miundombinu bora ya kilimo.
Alisema Katika serikali atakayoiongoza, ameahidi hatua madhubuti ili kuondoa changamoto hiyo na kuwafanya wakulima wawe wanufaika wa rasilimali zao.
Serikali ya ACT itaweka bei elekezi kwa bidhaa kama vanila, karafuu, pilipili hoho ili kuwalinda wakulima dhidi ya unyonyaji kutoka kwa madalali na walanguzi. Hili litahakikisha kuwa wakulima wanapata faida ya jasho lao.
Mamlaka hiyo itasimamia masuala yote ya uzalishaji, masoko, ubora, na usafirishaji wa viungo. Itasaidia kuunganisha wakulima na wanunuzi wa kimataifa kwa mikataba ya moja kwa moja.
Serikali itajenga viwanda vidogo vya kusindika viungo Pemba ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kwenda sokoni.
Akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia wakulima kupata bei nzuri zaidi na ajira kwa vijana.
Kupitia ushirikiano wa kimataifa, serikali itatafuta masoko ya uhakika kwa wakulima wa Pemba.
Othman ametolea mfano Nchi kama Madagascar huingiza mamilioni ya dola kila mwaka kupitia mauzo ya vanila, Zanzibar inaweza kufanya zaidi kwa kutumia ardhi yenye rutuba na hali ya hewa bora.
Othman alieleza kuwa Serikali ya ACT itahakikisha kuwepo kwa miundombinu ya umwagiliaji, pembejeo bora, na elimu ya kilimo ili kurahisisha uzalishaji na kuongeza tija.
Pia Othman aliainisha kuwa kilimo cha viungo kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi, anaonyesha dira mpya ya uongozi inayoeleweka kwa wananchi wa kawaida.
Hata hivyo alisema kwa muda mrefu, Pemba imekuwa na rasilimali nyingi lakini wananchi wake hawajanufaika kutokana na mifumo kandamizi ya kiutawala.
Kupitia hoja hizi, Othman anajenga ushawishi mkubwa wa kisiasa kwa kuwa anazungumzia matatizo halisi ya watu na kutoa suluhisho linalowezekana.
Sambamba na hayo alisema kwa wakazi wa Pemba, hasa wakulima, huu ni wakati wa kuchagua mabadiliko ya kweli. Kwa ACT Wazalendo, kura yao ni zaidi ya uchaguzi ni uwekezaji wa moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.
Wakulima wa eneo hilo walieleza kuwa wamekata tamaa na kilimo hicho kutokana na ukosefu wa masoko na gharama kubwa za uzalishaji.
Baadhi ya wakulima kama Bakari Mataka walisema licha ya kulima viungo kwa zaidi ya miaka 15, hajawahi kupata faida inayoweza kuihudumia familia yake kwa hata miezi mitatu.
Shabani Ali aliongeza kuwa wana mazao mengi nyumbani lakini hawajui pa kuyapeleka ili kupata bei nzuri na kurudisha gharama za uzalishaji.
Baada ya kusikiliza kwa makini hotuba ya Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, wakulima wa Shehia ya Mtambwe Daya walionekana kufarijika na kurudishiwa matumaini waliokuwa wameyapoteza kwa muda mrefu.
Hamza Sleiman amesema kauli yake ya kuwapa kipaumbele wakulima wa viungo na kulinda mazao yao kwa sera madhubuti iliibua hisia za matumaini na imani mpya kwa mustakabali wa maisha yao.
Wakulima hao walijadili kwa makundi namna ambavyo ahadi za kuwepo kwa masoko ya uhakika, bei elekezi, na viwanda vya kuchakata mazao zitaweza kubadili hali yao ya kiuchumi na kuinua maisha ya familia zao.
Pia wengine walieleza kuwa, kwa mara ya kwanza, walihisi kusikilizwa na kupewa thamani kama watu wanaochangia uchumi wa Zanzibar.
Wakiwa na nyuso zenye matumaini, wengi waliweka wazi kuwa wako tayari kumpa Othman Masoud ridhaa kupitia sanduku la kura, wakiamini ndiye kiongozi anayeelewa kwa undani changamoto zao na mwenye nia ya kweli ya kufanya mabadiliko ya msingi.
Kwao, uchaguzi wa Oktoba 29 si tukio la kisiasa tu, bali ni fursa ya kihistoria ya kuanzisha zama mpya ya maendeleo na heshima kwa wakulima wa Pemba. Waliahidi kumpigia kura kwa wingi, wakiamini kuwa sauti yao sasa imepata mtetezi wa kweli.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED