Sekta ya madini nchini inaendelea kushuhudia mageuzi makubwa ya kuongeza thamani si tu kwa madini ya vito na metali, bali pia kwa madini ya ujenzi kama mchanga. Mageuzi haya yamefungua fursa mpya kwa wachimbaji wadogo kupitia matumizi ya teknolojia bunifu za usindikaji.
Mkoani Tanga, kampuni ya Muwa Trading Tanzania Limited imewekeza katika kiwanda cha kuosha na kusafisha mchanga kwa kutumia maji, hatua inayosaidia kuondoa udongo na uchafu mwingine ikiwemo mizizi. Uwekezaji huu umebadilisha mtazamo wa thamani ya mchanga, ambao kwa miaka mingi uliuzwa kama malighafi ghafi isiyo na mnyororo wa thamani.
Kwa sasa, mchanga safi unaozalishwa mkoani Tanga unatumika kama malighafi ya uhakika kwa viwanda vya saruji, pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati ya Serikali ikiwemo ukarabati wa Bandari ya Tanga na ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika Kata ya Chongeleani.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Laurent Bujashi, alisema mchanga huo umekuwa chachu ya maendeleo ya viwanda na ujenzi.
“Mchanga unaosafishwa kiwandani hapa umetumika katika miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ukarabati wa Bandari ya Tanga, ujenzi wa baadhi ya viwanda, pamoja na utekelezaji wa bomba la mafuta ghafi kutoka Chongeleani. Hatua hii si tu kwamba imerahisisha upatikanaji wa malighafi zenye ubora, bali pia imefungua soko jipya kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa mchanga,” alisema Bujashi.
Kwa upande wake, Afisa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Kaparata Maulid, alisisitiza mchango wa teknolojia hiyo katika kukuza uchumi wa taifa:
“Kupitia teknolojia hii tumefanikisha kutoa mchanga wenye ubora wa hali ya juu unaokidhi mahitaji ya miradi mikubwa ya kimkakati nchini. Hii ni hatua muhimu katika kuongeza thamani rasilimali zetu na kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda.”
Kaparata alitaja manufaa ya mchanga uliosafishwa kuwa ni pamoja na:
Kupitia uwekezaji huu, Mkoa wa Tanga umejipambanua kama kitovu cha ubunifu na thamani katika sekta ya madini, ukiunga mkono dira ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda shindani kwa kutumia malighafi zinazopatikana ndani ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED