Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na kampuni ya SICPA Tanzania, imeanza kutoa mafunzo ya kitaifa juu ya matumizi ya programu mpya ya simu ya Smart DAS (Huisha Kidijitali), yenye lengo la kupunguza makosa ya kibinadamu na kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa kodi kwa walipakodi na wasimamizi wa sheria za kodi.
Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam, Meneja wa Mradi wa Stempu za Kielektroniki (ETS) kutoka Idara ya Mapato ya Ndani TRA, Abyud Tweve, alisema kuwa programu hiyo inayopatikana kwenye mifumo ya Android na iOS inaleta suluhisho rahisi na la kisasa kwa walipakodi nchini.
“Badala ya kuingiza kwa mkono namba za mfululizo wa stempu — mchakato uliokuwa na uwezekano mkubwa wa makosa — wazalishaji sasa wanaweza kuchanganua (scan) stempu ya kwanza na ya mwisho katika kila kifurushi. Programu hukusanya taarifa zote moja kwa moja na kuziwasilisha kwa mfumo wa TRA, hivyo kupunguza muda wa kutangaza na kuongeza usahihi wa taarifa,” alisema Tweve.
Alibainisha kuwa Smart DAS ni jibu la moja kwa moja kwa changamoto walizowasilisha walipakodi, na sasa inarahisisha uzingatiaji wa sheria za kodi sambamba na kuongeza uwezo wa TRA wa kusimamia uzalishaji kwa muda halisi.
Kwa mujibu wa Tweve, mafunzo ya awali yalihusisha maafisa 92 wa ETS na Vifaa vya Kielektroniki vya Kodi (EFD) kutoka mikoa mbalimbali. Maafisa hao walipata mafunzo ya kina juu ya matumizi ya programu hiyo pamoja na mbinu za kuiunganisha na mifumo mingine ya usimamizi wa kodi.
Katika hatua ya kuongeza uelewa wa kitaifa, kila afisa anatarajiwa kuratibu warsha kwa walipakodi kwenye mikoa yao ili kuhakikisha matumizi sahihi ya teknolojia hiyo mpya bila kuvuruga shughuli za uzalishaji.
Naye Meneja Mkuu wa SICPA Tanzania, Alfred Mapunda, alisema kuwa kampuni hiyo imetoa validator cards 5,000 kwa TRA, ambazo zitasaidia wauzaji wa jumla, wasambazaji na wadau wengine katika mnyororo wa bidhaa za ushuru kuhakikisha uhalali wa stempu kabla ya bidhaa kukubaliwa sokoni.
“SICPA Tanzania inajivunia kushirikiana na TRA katika kuimarisha usimamizi wa kodi kupitia teknolojia salama na bunifu. Kadi za uhakiki na Smart DAS ni sehemu ya dhamira yetu kusaidia Tanzania katika safari ya usimamizi wa kodi wa kisasa, wa uwazi na wa kuaminika,” alisema Mapunda.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo ni hatua kubwa katika kulinda mapato ya serikali kupitia mfumo wa ushuru wa bidhaa, huku ukihamasisha uzingatiaji wa kodi kwa hiari kwa kutumia teknolojia rafiki kwa watumiaji.
Mapunda alihitimisha kwa kusema kuwa Tanzania inaendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika matumizi ya suluhisho za kidijitali kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato, sambamba na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Kenya na Uganda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED