Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Youth Coalition (TYC) limewahimiza vijana nchini kuangalia kwa jicho la pili sekta ya kilimo, likisema kuwa sekta hiyo imejaa fursa lukuki za ajira kuanzia hatua ya uzalishaji mashambani hadi kwenye mnyororo wa thamani viwandani na masokoni.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Mradi wa YEFA Kilimo Sauti, Josephina Onesmo, mara baada ya majadiliano maalum na vijana kuhusu fursa na changamoto katika kilimo biashara.
Onesmo amesema changamoto ya ajira imeendelea kuwa kubwa kwa kundi la vijana, lakini suluhisho linaweza kupatikana endapo vijana wataamua kubadili mtazamo kuhusu kilimo.
“Vijana ni kundi kubwa lenye nguvu kazi nchini lakini ndilo linaloathirika zaidi na ukosefu wa ajira. Wengi wao wanaamini kuwa kilimo ni kazi ya watu wasiosoma, jambo ambalo si kweli. Kilimo kina fursa nyingi na kinaweza kutoa ajira zenye heshima na kipato cha uhakika,” amesema Onesmo.
Ameongeza kuwa kupitia mradi wa YEFA Kilimo Sauti, TYC inalenga kuwawezesha vijana kufahamu na kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa kilimo biashara, sambamba na kuwajengea uwezo wa kuanzisha miradi yao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
TYC imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa vijana katika maendeleo kupitia miradi mbalimbali, huku ikisisitiza kuwa kilimo si tu chanzo cha chakula, bali pia ni njia madhubuti ya kujenga uchumi wa vijana na taifa kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED