SERIKALI Wilaya ya Mkuranga, imewataka wafugaji wa nyuki kubadili mitazamo yao na kujikita kuongeza thamani, kwa kile wanachozalisha, ili kupata fedha nyingi zaidi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga, Omary Mwanga, ametoa wito huo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Nyuki, yaliyofanywa na wilaya hiyo na kuvikutanisha vikundi mbalimbali vya wafugaji nyuki.
Mwanga amesema wafanyabiashara wa zao la nyuki wanashauriwa kuongeza thamani ya biashara zao na kubadili mtazamo wao kwa kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha, ili kipato wanachopata kiongozeke.
"Isiwe tu ni asali hata yale yanayopatikana kwenye asali tuweze kuyatumia wafanyabiashara wayaweke kwenye mpango wao kuyaongezea thamani tuongeze uzalishaji na ubunifu, ili tuendelee kujidhatiti katika ushibdani wa biashara," amesema.
Katibu Tawala huyo amesema, ni vema kubadilisha mfumo wa maadhimisho kama hayo, ili yaweze kuwa na tija kwa washiiriki na kuwa kikao kazi na kutengeneza maazimio ya namna ya kuinua ufugaji.
Amesema maadhimisho kama hayo wataalamu wanatakiwa kupata fursa ya kutoa ujuzi kwa wafugaji nyuki, ili kuboresha shughuli zao na kuwaletea mabadiliko ya kiuchumi.
Awali Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi na Utunzaji Misitu Wilaya ya Mkuranga, Asted William, amesema kwa kipindi cha miaka mitano wamefanikiwa kuwa na mizinga ya kisasa 1,015 na mizinga ya kienyeji 72 yote ikizalisha kilo 3000 sawa na tani tatu hadi.
Kitengo hicho kimemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa namna alivyotoa kipaumbele kwa ufugaji nyuki kwa kuhakikisha anatengeneza mazingira yaliyowezesha asali yao kuuuzwa masoko ya nje ya nchi ikiwemo China na nchi nyingine duniani.
Sambamba na hilo, amesema Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mkutano mkubwa unaowakutanisha wadau wa ufugaji nyuki duniani.
Kwa mujibu wa Asted, kwa sasa wanakabiliwa na tatizo la mabadiliko ya tabianchi, yanayochangiwa na uchomaji wa moto mizinga na mbinu za uvunaji zisizo za kitaalamu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED