Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi ameeleza kufurahishwa kwake na mjasiriamali aliyenufaika na mafunzo ya kuendeleza ujuzi kupitia Mfuko wa SDF wa Mamlaka ya Elimu Tanzania TEA.
Esther Shebe ambaye amenufaika na mafunzo ya kuendeleza ujuzi kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) anavyotengeneza bidhaa mbalimbali.
Ameyasema hayo leo wakati alipotembelea TEA kwenye hafla ya kufunga maonyesho ya kitaifa ya kazi za utamaduni na Sanaa yaliyokuwa yakifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akiwa kwenye banda hilo baada ya kusikiliza mafanikio ya mjasiriamali huyo, Waziri Kabudi aliwataka watanzania wasiogope kufanya ujasiriamali wa Kilimo kwani wanaweza kunufaika kama Shebe ambaye amemudu kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na Uyoga.
“Nimefurahi sana kuona namna ulivyoweza kutengeneza bidhaa nyingi kwa kutumia uyoga nahamasiha na wengine wafanye kama wewe wajiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa namimi naahidi nitakuwa mteja wako,” amesema kabudi
Shebe anayemiliki kampuni ya Goba Mushroom Zone, alimweleza Waziri kuwa kupitia kilimo cha uyoga amepata mafanikio makubwa ikiwemo kupata tuzo ya kuwa malkia wa nguvu na mkulimo bora wa mwaka 2021.
Amesema yeye alikuwa mkulima kwa miaka mingi lakini mwaka 2022 alikwenda kuongeza ujuzi kupitia Mamlaka ya Kuwendeleza Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) kupitia mfuko wa SDF ambayo yamemwezesha kutengeneza bidhaa mbalimbali.
“Natengeneza bidhaa mbalimbali kutokana na uyoga, nina maabara yangu ambayo naitumia kutengeneza mbegu za uyoga ambazo nauza na zingine nazipanda kwenye shamba langu mwenyewe,” amesema
Amesema mwaka 2023 alipata cheti cha mkulima bora Mkoa wa Dar es Salaam Kanda ya Mashariki na mwaka 2024 alipata tuzo ya kampuni bora ya kilimo na aliishukuru TEA kwa namna ilivyomwezesha kupata mafunzo ambayo yamempa mafanikio makubwa.
“Niliwahi kwenda China kwa mafunzo ya muda mfupi kuongeza ujuzi kupitia chuo cha Sokoine cha Morogoro. Watu wasiogope kilimo kinalipa kwasababu mimi nilikuwa nimeajiriwa Napata mshahara ambao ulikuwa hautoshi lakini kipato changu kwa sasa kinatosheleza mahitaji yangu,” amesema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED