Baltasar Engonga ahukumiwa miaka minane jela kwa ubadhirifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:26 PM Aug 28 2025
Baltasar Engonga.
Picha:Mtandao
Baltasar Engonga.

Mahakama ya Mkoa wa Bioko, nchini Equatorial Guinea, imemhukumu Baltasar Ebang Engonga, mkuu wa zamani wa Shirika la Taifa la Upelelezi wa Masuala ya Kifedha (NFIA), kifungo cha miaka minane jela baada ya kupatikana na hatia ya ubadhirifu wa fedha za umma na kujipatia mali kinyume cha sheria.

Engonga, ambaye ni mpwa wa Rais Teodoro Obiang Nguema, alihukumiwa pamoja na maafisa wengine watano waandamizi waliopatikana na hatia ya kuiba mamia ya maelfu ya dola kutoka hazina ya taifa na kutumia fedha hizo kwa maslahi binafsi.

Mahakama pia imewapiga faini kubwa, ambapo Engonga anatakiwa kulipa dola 220,000, huku washirika wake wakipewa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja.

Baltasar Ebang Engonga alikuwa miongoni mwa watu waliodhaniwa kuwa na nafasi ya kurithi urais kutoka kwa Obiang Nguema, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1979 na kwa sasa ana umri wa miaka 82. Hata hivyo, hukumu hii inachukuliwa kama pigo kubwa kwake na ishara ya changamoto za uwajibikaji serikalini katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta, lakini linalokabiliwa na kashfa za kifedha mara kwa mara.

Mbali na mashtaka ya kifedha, Engonga pia amejipatia umaarufu wa aibu kufuatia kuvuja kwa video kadhaa za ngono mitandaoni, zinazodaiwa kumhusisha na wake wa maafisa wengine wa serikali. Tukio hilo limeongeza zaidi doa katika taswira yake ya kisiasa na kijamii.