Waumini 2,000 wahitimu mafunzo ya ufugaji kuku

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 02:03 PM Aug 29 2025
Waumini 2,000 Wahitimu Mafunzo ya Ufugaji Kuku, Wapongezwa kwa Kujikwamua Kiuchumi.
Picha: Imani Nathaniel
Waumini 2,000 Wahitimu Mafunzo ya Ufugaji Kuku, Wapongezwa kwa Kujikwamua Kiuchumi.

Mkurugenzi wa Sab Investment, Saida Bwanaheri, amewapongeza waumini wa Kanisa la Christ Mandate and Power Ministries International kwa kuhitimu mafunzo ya ufugaji wa kuku, akisema hatua hiyo ni msingi wa kujikwamua kiuchumi na kupunguza utegemezi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya mafunzo hayo, yaliyohusisha zaidi ya wahitimu 2,000, Bwanaheri alisema viongozi wa dini wanapaswa kuhamasisha waumini wao kushiriki katika shughuli za kimaendeleo badala ya kuishia kwenye ibada pekee.

“Ni muhimu taasisi za kidini zisionekane tu katika ibada, bali ziwe chachu ya kuhamasisha waumini kushiriki shughuli za kiuchumi kama ufugaji, ili kupunguza ugumu wa maisha,” alisema.

Ujuzi wa Kujitegemea

Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Sab Investment, Charles Kimario, alisema tukio la kuwatunuku vyeti wahitimu litawasaidia vijana kujiondoa kwenye utegemezi na kujipatia kipato kupitia sekta ya ufugaji.

“Tunatoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa za ufugaji wa kuku kwani sekta hii ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema Kimario.

Naye Dariana Mushi, Balozi wa Sab Investment, alisema mafunzo hayo si tu kwamba yatawanufaisha wahitimu, bali pia yatachangia mageuzi chanya katika sekta ya ufugaji nchini.

“Tunawapongeza viongozi wa kanisa hili kwa kuruhusu waumini wao kushiriki mafunzo yenye manufaa ya moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku,” alisema.