Mke wa Rais wa zamani Korea Kusini akamatwa kwa utapeli na hongo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:45 PM Aug 13 2025
Mke wa rais wa zamani wa Korea Kusini, Kim Keon Hee.
Picha: Mtandao
Mke wa rais wa zamani wa Korea Kusini, Kim Keon Hee.

Mke wa rais wa zamani wa Korea Kusini, Kim Keon Hee, amekamatwa na kuzuiliwa kutokana na mashtaka kadhaa, ikiwemo utapeli wa mali na kupokea hongo.

Kim, ambaye ni mke wa rais wa zamani Yoon Suk Yeol aliyeko gerezani, alikanusha mashtaka hayo yote wakati wa kusikilizwa kwa kesi iliyodumu saa nne katika mahakama ya Seoul, Jumanne hii. Hata hivyo, mahakama iliamua kutoa hati ya kizuizi ikibainisha uwezekano wa kuharibu ushahidi.

Korea Kusini imezoea marais wa zamani kufunguliwa mashtaka na kufungwa jela, lakini hii ni mara ya kwanza kwa rais wa zamani na mke wake wote kuwa gerezani kwa wakati mmoja.

Yoon alikamatwa Januari mwaka huu akikabiliwa na kesi ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindikana mwaka jana, hatua iliyosababisha machafuko nchini na hatimaye kumng’oa madarakani.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, Kim (52) anadaiwa kupata zaidi ya ₩800 milioni ($577,940; £428,000) kwa kushiriki mpango wa udanganyifu wa bei za hisa za Deutsch Motors, muuzaji wa magari ya BMW nchini humo. Matukio hayo yanadaiwa kutokea kabla ya mumewe kuchaguliwa kuwa rais, lakini yameendelea kuibua sintofahamu wakati wote wa uongozi wake.

Aidha, Kim anatuhumiwa kupokea mifuko miwili ya Chanel na mkufu wa almasi kama hongo kutoka Kanisa la Muungano, lenye historia ya utata, ili kubadilishana na msaada wa kibiashara.

Mashtaka mengine yanayomkabili ni pamoja na kuingilia mchakato wa uteuzi wa wagombea wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge mwaka 2022 na uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Alipofika mahakamani Jumanne, Kim alionekana mtulivu, akiwa amevalia suti na sketi nyeusi. Akizungumza kwa kifupi na waandishi wa habari, alisema:

“Ninaomba msamaha wa dhati kwa kusababisha matatizo, licha ya kuwa mtu asiye na umuhimu.”