RAIS wa Kenya William Ruto ametofautiana na waziri wake baada ya kulihakikishia taifa kuwa serikali yake imejitolea katika kufadhili sekta ya elimu.
Wakati huo huo, Waziri wa Hazina ya Kitaifa John Mbadi amesema serikali haina fedha za kutosha kufadhili kikamilifu elimu ya bure kwa shule za upili.
Waziri huyo alienda mbali zaidi na kubainisha kuwa KSh 5,344 zinazotolewa kama mgao kamili wa fedha za karo kwa kila mwanafunzi zimepunguzwa, hali ambayo imeibua ghadhabu ya wananchi nchini humo.
Akizungumza mbele ya kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu elimu, Mbadi ameeleza kuwa wanafunzi wa shule za upili pia watapunguziwa mgao wao kutoka KSh 22,244 hadi KSh 16,900 kwa kila mwanafunzi.
Julai 27, mwaka huu Rais Ruto alithibitisha kujitolea kwa utawala wake kutoa elimu bila malipo, na elimu bora kwa watoto wote wa Kenya.
Alisisitiza uwekezaji unaoendelea wa serikali ya Kenya Kwanza juu ya kupanua ufikiaji wa elimu na kuboresha hali ya masomo.
Ruto amebainisha kuwa utawala wake umetenga fedha nyingi kusaidia elimu tangu aingie madarakani 2022.
“Tumeweka fedha nyingi katika sekta ya elimu ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma, pia tumeongeza ufadhili kwa vyuo vikuu na kuajiri walimu zaidi ya 70,000 katika miaka miwili iliyopita. Tunapanga kuajiri walimu 24,000 zaidi ifikapo mwanzoni mwa mwaka ujao,” Rais alisema.
Akitoa mfano wa hivi karibuni wa kutiwa saini kwa Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja (CBA) kati ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) na chama cha walimu, utakaodumu hadi 2029, Ruto alishikilia kuwa serikali yake imedhamiria kudumisha uthabiti katika sekta ya elimu.
Rais ameihakikishia nchi kuwa amejitolea kufanya elimu sio tu ya bei nafuu na ya kujumuisha wote bali pia ya ubora mzuri na inayofaa mahitaji ya maendeleo ya Kenya.
“Ninawahakikishia kuwa upatikanaji na ubora wa elimu hauwezi kuathiriwa,” ameongeza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED