Tume ya Uchaguzi Cameroon yamzuia mpinzani wa Rais Biya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:38 AM Jul 28 2025
Mwanasiasa wa upinzani Maurice Kamto.
Picha: Mtandao
Mwanasiasa wa upinzani Maurice Kamto.

Tume ya uchaguzi ya Cameroon, ELECAM, imetangaza kuwa mwanasiasa wa upinzani Maurice Kamto amezuiliwa kushiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais wa Oktoba 12 mwaka huu.

Profesa, huyo mashuhuri wa chuo kikuu na waziri wa zamani wa serikali anaonekana kuwa ndiye mshindani mkuu wa rais wa muda mrefu wa nchi hiyo Paul Biya.
 
ELECAM imesema, Kamto alishindwa kufuata matakwa ya kisheria kwa kukubali kuteuliwa kuwa mgombea wa vuguvugu la Cameroon Renaissance, ambalo lilisusia uchaguzi wa wabunge na manispaa mnamo mwaka 2020.
 
Kwa mujibu wa tume hiyo, kwa kuzingatia Kifungu cha 121 cha kanuni za uchaguzi, hatua hiyo ya kususia uchaguzi, imelifanya vuguvugu hilo lisiwe tena na ustahiki wa kuweka mgombea katika uchaguzi.
 
Kamto alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 14 ya kura katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2018, ambao Biya alishinda kwa kishindo huku kukiwapo na madai ya kufanyika udanganyifu.
 
Kuenguliwa mtiania huyo mwenye umri wa miaka 71 kunaongeza hatari ya kuzuka malalamiko na kubakisha waombaji 12 tu kati ya zaidi ya watarajiwa 80 wa kuchukua nafasi ya Biya mwenye umri wa miaka 92 .
 
Akiwa yuko madarakani kwa takribani miaka 43, Paul Biya alitangaza mapema mwezi huu kwamba atawania muhula wa nane wa miaka mingine saba ya kuendelea kubaki madarakani.

Rais wa Cameroon Paul Biya.