UINGEREZA na mataifa mengine ya Ulaya, yanatarajiwa kukutana na nafasi yao kubwa zaidi leo kuliko ilivyokuwa Alaska.
Viongozi kadhaa wa Ulaya wametangaza kuwa watajiunga na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, katika ziara ya Ikulu ya White House, leo Jumatatu.
Waliothibitisha kushiriki mkutano huo ni Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer; Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Melon; Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz; Rais wa Finland Alexander Stubb; Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron; Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte na Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen,
Hata hivyo, Zelensky alikutana na von der Leyen, huko Brussels, kabla ya mkutano wa mtandaoni na viongozi kadhaa wa Ulaya.
Rais Zelensky yuko Washington, leo kwa mara ya kwanza tangu alipokemewa hadharani Februari mwaka huu na Rais Trump pamoja na Makamu wa Rais Vance.
Dunia inaelekeza jicho huko kutazama tukio hilo kwa mshangao.
Haijawahi kutokea Ikulu ya Oval au hata katika historia ya diplomasia ya kimataifa.
Zelensky alifukuzwa White House. Ilionekana vigumu kufikiria kurekebisha uhusiano huo. Lakini katika miezi iliyofuata, viongozi wa Ulaya walifanya kazi kwa bidii nyuma ya pazia kuusuka upya.
Kiongozi wa Ukraine alipewa mafunzo ya kutumia lugha ya kumfurahisha Trump, kuzungumza kuhusu mikataba na biashara.
Mazungumzo bado rasmi ni kati ya Rais Trump na Zelensky, lakini viongozi wengine akiwamo Keir Starmer, wanatumaini uwapo wao Washington utatoa ishara madhubuti kuwa Ulaya ipo upande wa Ukraine.
Waziri Mkuu Starmer, alijua ni vigumu kushuhudia tukio la Februari kati ya Trump na Zelensky katika Ikulu ya Oval.
Tangu wakati huo ameonesha nia ya kumsaidia Zelensky kupita salama katika mazingira ya White House, inayoongozwa na Trump.
Starmer amefanya kazi kwa bidii kudumisha uhusiano wa karibu na Trump.
Ziara yake White House Februari ilikuwa ya kirafiki, vivyo hivyo na ziara ya Trump Scotland.
Pamoja na Rais wa Finland Alexander Stubb, Starmer anaonekana kuwa kiongozi wa Ulaya aliye karibu zaidi na Rais wa Marekani.
Kuna imani kubwa Downing Street kwamba uwapo wa Starmer kwenye matukio kama haya unaweza kusaidia akawa kiungo kati ya Trump na Zelensky.
Kumudu tabia ya Donald Trump ni sehemu ya operesheni ya kidiplomasia, hasa ikizingatiwa yaliyojiri katika ziara ya mwisho ya Zelensky Washington.
Kwa sasa, tukio la kipekee – idadi kubwa ya viongozi wa “muungano wa walio tayari” wamethibitisha kushiriki mkutano White House.
Lengo kuu litakuwa kushinikiza hitaji la dhamana za usalama kwa Ukraine baada ya mkataba wa amani, kwa kuwa uanachama wa NATO kwa Ukraine bado si suala lililo mezani.
Pia, viongozi hao watataka kuibua ‘masuala ya mipaka’ na Trump na kusisitiza uungaji mkono wao kwa Ukraine.
Mkutano uliopangwa awali kuwa wa wawili kati ya Trump na Zelensky sasa unaonekana kupanuka – ingawa huenda bado wakaonana faraghani, huku viongozi wengi wa Ulaya wakielekea White House, kwa ajili ya kikao cha pamoja na Rais wa Marekani.
Wale walio na uhusiano mzuri na Trump wamekuwa wakifanya jitihada kupata fadhila kwa niaba ya Zelensky, hasa tangu kikao cha chemchemi White House.
Kwa hali ilivyo, huu ni mkutano wa aina yake. Ni vigumu kukumbuka mara nyingine ambapo viongozi wengi wa Ulaya kwa muda mfupi sana waliamua kuvuka Atlantiki kushinikiza suala fulani.
Ni wazi kuna wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Ulaya baada ya mkutano wa Alaska kati ya Trump na Putin na ndiyo maana wanakwenda kwa wingi kufikisha ujumbe wao kwa Rais wa Marekani.
TRUMP
Wakati viongozi wa Ulaya wanakutana tena na Rais Zelensky, Trump amechapisha taarifa kadhaa katika mtandao wake wa kijamii ukiwamo wa Truth Social, akisema;
“Maendeleo makubwa kuhusu Russia...endelea kufuatilia!,” unasomeka ujumbe huo.
“Nilikutana vizuri sana kule Alaska kuhusu vita vya kijinga vya Biden, vita ambavyo havikupaswa kabisa kutokea!!!”
Mwishoni mwa wiki, Rais Trump alipokutana na Putin alisema wamekuwa na mkutano wenye tija na kwamba wamepiga hatua kubwa.
Trump na Putin walizungumza kwa pamoja jukwaani kwa takriban dakika 10.
Wote wawili walionesha ishara ya mazungumzo mema waliokuwa nayo wakati wa mkutano wao wa faragha, ingawa ulimalizika bila makubaliano madhubuti.
Putin alisema ana nia ya dhati katika kukomesha mzozo huo, ambao alielezea kuwa janga.
Lakini alisema, Russia inahitaji sababu za msingi" za mzozo huo zitatuliwe kwanza na akaonya Ukraine na Ulaya hazipaswi kuhujumu mazungumzo hayo.
Trump alimalizia kwa kusema kuna uwezekano mkubwa ataonana tena na kiongozi wa Russia hivi karibuni, huku Putin akijibu kuwa: "Wakati ujao itakuwa Moscow."
ZELENSKY ANATARAJIA MAKUBWA
Zelensky anatarajia ziara yenye matokeo Ikulu ya White House. Akiwa katika mkutano wa waandishi wa habari kutoka Ukraine, akimwuliza Zelensky ni aina gani ya dhamana za kiusalama angeona zinafaa, na kama ana hofu ya kurudiwa kwa mabishano makali yaliyotokea Ofisini kwa Oval wakati wa ziara yake ya Februari.
Zelensky alijibu kuwa anaelewa ufadhili wa dhamana za kiusalama unaweza kufanywa na Ulaya pekee, lakini bado kuna mambo ambayo Marekani inaweza kutoa.
Amesema pia Ukraine inahitaji dhamana kwamba Russia, haitandelea kuikalia nchi jirani.
Kuhusu ziara yake White House, amesema anatarajia kuwa itakuwa yenye matokeo chanya.
Zelensky amesema kuwa “Putin ana madai mengi lakini bado hatuyajui yote,” na kuongeza kuwa itachukua muda kuyapitia yote, iwapo yapo kwa wingi kama inavyosemwa.
Amesema haiwezekani kufanya hivyo sasa chini ya shinikizo la mapigano, hivyo kunahitajika usitishaji mapigano ili kufanya kazi haraka kuelekea makubaliano ya mwisho.
Kwa matokeo hayo, amesisitiza kuwa “mazungumzo ya kweli” yanayojikita pale mstari wa mapigano ulipo sasa ndiyo yanahitajika.
Ameongeza tena kuwa katiba ya Ukraine haiwezi kuruhusu kuachia ardhi na jambo hilo linapaswa kujadiliwa tu na viongozi wa Ukraine na Russia katika mkutano wa pande tatu.
Zaidi, amesema ni muhimu Marekani ikubaliane kutoa dhamana za kiusalama kwa Ukraine sambamba na Ulaya.
“Tunahitaji usalama ufanye kazi kwa vitendo kama Ibara ya 5 ya NATO,” ameongeza, akirejelea agizo la NATO kuwa wanachama wake watasaidia mwanachama yeyote atakayeshambuliwa.
MAKALA HII IMEANDALIWA KWA MSAADA WA VYOMBO KIMATAIFA
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED