ACT Wazalendo yasisitiza mshikamano na CHADEMA, yaionya polisi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:17 PM Mar 26 2025
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu

Chama cha ACT Wazalendo kimesema hakiwezi kunyamaza kimya endapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kitapitia changamoto au kukandamizwa, kikisisitiza mshikamano wake na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha ndani cha chama hicho wilayani Kilwa, mkoani Lindi.

Ado Shaibu, amesema chama chake hakiwezi kufumbia macho matukio yanayoikumba CHADEMA, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa mikutano yao ya hadhara na kutoweka kwa baadhi ya viongozi wao.

"Baadhi ya watu wametuhoji kwa nini ACT inakuwa sauti ya CHADEMA. Leo nataka niwaambie Wanakilwa, ikiumizwa CHADEMA tukakaa kimya, anayefuata ni nani? Ni sisi ACT Wazalendo. Ikiumizwa CHADEMA tuchukulie kwamba tumeumizwa na sisi," amesema Ado Shaibu.

AITUHUMU POLISI KWA UPENDELEO

Shaibu pia amelikosoa Jeshi la Polisi kwa kile alichokiita ubaguzi wa wazi katika utoaji wa ulinzi kwa vyama vya siasa. Ameeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapewa ulinzi mkubwa, huku mikutano ya vyama vya upinzani ikizuiwa bila sababu za msingi.

"Tunafahamu kuwa viongozi wao wawili hawaonekani mpaka sasa katika kipindi cha wiki chache zilizopita. Tunafahamu pia kuwa jeshi la polisi limezuia mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliopangwa kufanyika Machi 25, 2025, kule Mbarali, Mbeya. Ninawaambia ndugu zetu wa CHADEMA tupo pamoja, tutashirikiana, na tunalionya jeshi la polisi kwa kufanya kazi kwa ubaguzi," amesema.

Ado Shaibu amehoji ni kwa nini mikutano ya CCM inapewa msukumo wa magari ya polisi hadi kubeba watu huku mikutano ya upinzani ikiwa na vikwazo na marufuku zisizoeleweka.