Simba yapewa mbinu kuimaliza Al Masri

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:47 PM Apr 01 2025
Wachezaji wa kikosi cha Simba katika mazoezi Misri
Picha: Mtandao
Wachezaji wa kikosi cha Simba katika mazoezi Misri

MCHEZAJI na kocha wa zamani wa Simba, Talib Hilal, ametoa mbinu ambazo zinaweza kuifanya timu hiyo kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Masry, unaotarajiwa kuchezwa kesho, saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa New Suez, nchini Misri.

Akizungumza kutoka nchini Oman, ambako ndiko anakoishi kwa sasa, Talib, aliyeichezea Simba mwishoni mwa miaka 1980 hadi mwanzoni mwa 1990, amemshauri Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids kumuanzisha, Leonel Ateba mbele na kumpa maelekezo Elie Mpanzu kuacha kukaa na mpira muda mrefu na kufanya vitu visivyo na maana.

Talib, ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa Simba kuivua taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek ya Misri mwaka 2003, alipoteuliwa kuwa mmoja wa jopo la makocha lililochangia timu hiyo kutinga hatua ya makundi mwaka huo, pia aliwataka mabeki wa timu hiyo wasiwe na mambo mengi wanapokuwa kwenye eneo la hatari.

"Kwenye ushambuliaji nadhani Ateba anafaa pale mbele kwa sababu ushirikiano wake na viungo washambuliaji umekuwa mzuri kwa siku za hivi karibuni, na sidhani kama atakibadili kikosi chake, nina imani atapanga kile kile anacho kuwa anakipanga.

 Mpanzu ajaribu kutumia kasi yake na uwezo wa kukokota mpira, lakini apunguze vitu ambavyo havina faida hasa ugenini ambako timu inahitaji zaidi matokeo au mabao kuliko kitu kingine chochote, asikae sana na mpira, watu hawawezi kukuachia, lakini ni mchezaji mzuri anayeweza kuchangia ushindi wa Simba," alisema Talib ambaye alikuwa akicheza beki wa kati enzi zake.

Aliwaonyesha baadhi ya mabeki wa Simba kuwa na tabia ya kujiamini kupita kiasi, akisema itawagharimu.

"Mabeki wa Simba wacheze kwa kujiamini na kucheza mipira rahisi, beki anatakiwa kurahisisha kazi yake, asiifanye kazi ikawa ngumu, ukiwa beki hutakiwi kujiamini kupita kiasi, kosa moja linaweza kusababisha madhara, nataka mabeki wacheze kama Abdulrazack Hamza, hana mambo mengi, anajiamini na anacheza mipira rahisi," alisema.

Akiizungumzia kwa ujumla mechi hiyo ya mkondo wa kwanza, alisema itakuwa ngumu, lakini kama Simba watacheza kama alivyokuwa akiwaona kwenye michezo ya nyuma, inaweza kushinda au kutoa sare, huku akisifu mbinu za Fadlu anapocheza akiwa ugenini.

"Mechi ni ngumu, kama unavyojua timu za Misri zinajua sana kutumia viwanja vyao vya nyumbani, pamoja na hayo nadhani zamani ndiyo walikuwa wanazitisha timu kutoka nchi zingine, siku hizi nazo zimejanjaruka na zinajua mbinu wanazotumia, pia Simba si mara ya kwanza kucheza nchini Misri.

Najua mechi hii itakuwa ngumu pia kwa sababu timu wanayocheza nayo ni nzuri sana, lakini nina imani kwa jinsi ilivyo Simba kwa sasa inaweza kupata ushindi ikiwa ugenini," alisema Talib.

Aidha, alisema Fadlu ana uzoefu wa soka la Kiafrika hasa wakicheza ugenini, kama walivyocheza mechi za makundi.

Simba imeondoka leo Ismailia kwenda kwenye mji wa Canal ambako ndiko mchezo huo utachezwa kesho, marudiano ya mechi hiyo yatakuwa Aprili 9 kwenye  uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.