Wachezaji Yanga waapa kulipiza kisasi Tabora

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:41 PM Apr 01 2025
Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi
Picha: Mtandao
Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi

NI mechi ya kisasi!, ndivyo unaweza kusema wakati Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, watakaposhuka leo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, kujaribu kulipa kisasi dhidi ya Tabora United, huku wachezaji wa timu hiyo, wakisema wamekwenda mkoani huko kwa mambo mawili, kisasi na kuchukua pointi tatu.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, amesema wamejiandaa vizuri na wapo tayari kwa mchezo huo na kuchukua pointi tatu.

"Walitusumbua kweli, walitufunga mabao matatu, kwa sasa tupo vizuri, nawaambia Tabora United kwa niaba ya wachezaji wenzangu, walikuja kwetu, lakini sasa tupo kwao, pointi tatu tunazitaka, tumejipanga vizuri kulipiza kisasi," alisema Mwamnyeto.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu uliopigwa, Uwanja wa Azam Complex Novemba 7 mwaka jana, Dar es Salaam, Yanga ilikutana na kipigo cha kushtukiza cha mabao 3-1 dhidi Tabora United.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miloud Hamdi, amesema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na kucheza na timu ambayo ilipata ushindi kwenye mchezo wa kwanza, hivyo watajitutuma, lakini wao wamejipanga kuonyesha kwamba ni timu kubwa.

"Yanga ni timu kubwa, tunakwenda kucheza mechi ngumu, timu hii ilipata ushindi mchezo uliipita, safari hii tumejipanga kuwapa furaha wanachama na mashabiki wa Yanga, nadhani watajitokeza kwa wingi kama kawaida yao kuwapa sapoti wachezaji kama ambavyo huwa wanafanya kwenye michezo yote," alisema kocha huyo.

Wachezaji Tabora waahidiwa mamilioni

Kwa upande wa Tabora United, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, ameahidi kitita cha Shilingi Milioni 60, kama timu hiyo itaibuka na ushindi dhidi ya Yanga.

Aliwataka wachezaji wa timu hiyo wakapambane, watoe tone la mwisho la jasho na damu kwa ajili ya Tabora United, lakini pia kwa ajili ya maisha yao ya soka ya baadaye kwani mechi kama hii inafuatiliwa na watu wengi.

"Nawaambia wachezaji wa Tabora United kuwa hiki ndicho kibarua chenu na asitokee mtu anacheza na kibarua chenu, mnajua kuwa tulitoa wachezaji watatu kwenda kwenye timu za taifa, kazeni, inawezekana yanayokuja ni mazuri zaidi, wapo wanaowadanganya, najua, wengine wanapitisha meseji, achaneni nazo, mtu akikupa pesa wala usiwe na mashaka, wewe chukua, kula, halafu fanya kazi yako, nyinyi bado vijana wadogo, na baada ya hapa mkipata matokeo mazuri nyinyi wenyewe mtaona matokeo mazuri huko mbele," alisema Chacha.

Alisema walitenga kiasi cha shilingi milioni 50 ambazo wangewapa wachezajikama wangeibuka ushindi kwenye mchezo dhidi ya Simba ambao hata hivyo walipoteza kwa mabao 3-0 Februari 2 mwaka huu

"Siku ile niliwaambia mkiwafunga Simba nitawapa Milioni 50, lakini haikuwa riziki, sasa ile pesa sijawahi kuitumia, niliiacha kwa makusudi kwa sababu nilijua kuna mechi dhidi ya Yanga hapa, kwa hiyo ile pesa ipo na nimeongeza milioni 10 zaidi, mkiubuka na ushindi mtapewa milioni 60.

Nitakuja uwanjani kuangalia mpira nikiwa na Milioni 60 mezani kwa ajili yenu, nyinyi kapambaneni, msimuogope mtu," alisema.

Yanga inashuka uwanjani leo ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 58, huku Tabora United ikikamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 37.