Afungwa maisha kumnajisi mtoto

By Jumbe Ismaily , Nipashe
Published at 02:00 PM Aug 28 2025
Jela
Picha: Mtandao
Jela

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida imemhukumu kifungo cha maisha jela Emmanuel Musa (27), mkazi wa kijiji cha Ighombwe, wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumnajisi binti wa darasa la tano (jina tunalo) katika shule ya Msingi Ighombwe.

Awali, Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Mkoa wa Singida, Nehemia Kilimhana, alidai kwamba Novemba 12, 2023 mshitakiwa akiwa katika Kijiji cha Ighombwe, alimnajisi binti mwenye umri wa miaka 13 ambaye ni mwanafunzi huyo uku akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Shauri hilo la jinai lililofunguliwa katika mahakama hiyo Aprili,11,2023 na kusajiliwa kwa namba 8699/2025 lilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Allu Nzowa.

Aliposomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikana ndipo upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wanne ambao walitoa ushahidi bila kuacha shaka yoyote kuwa huyo ndiye aliyetenda kosa hilo.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka huyo, mshtakiwa alijitetea mwenyewe na baada ya Mahakama kusikiliza pande zote mbili, ilimtia hatiani kwa kosa hilo la kunajii ili liwe fundisho kwa watu wenye tabia kama ya mshtakiwa.

Mahakama hiyo ilimhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumnajisi mwanafunzi huyo.