AG Johari: Wanasheria wawe walinzi wa sheria za mazingira

By Ibrahim Joseph , Nipashe
Published at 12:09 PM Sep 04 2025
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari
Picha: Ibrahim Joseph
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amewataka wanasheria kuongeza umakini na kuwa walinzi wa sheria zinazohusu mazingira kwa maslahi mapana ya taifa.

Johari alitoa wito huo, Septemba 3, 2025, wakati akifungua mafunzo kwa mawakili wa serikali kuhusu sekta ya mazingira yaliyofanyika jijini Dodoma, yakiandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC).

Amesema mafunzo hayo yatawasaidia mawakili hao kuelewa vizuri sheria na taratibu zinazohusu usimamizi wa mazingira, pamoja na kufahamu majukumu ya NEMC hususan kuhusu ada na tuzo za kisheria.

 Johari aliongeza kuwa elimu hiyo itawawezesha kutoa ushauri wa kisheria sahihi kwenye mikataba inayohusu hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.

Aidha, alibainisha kuwa serikali inaendelea kufanya tathmini ya mifumo ya kitaasisi kwa lengo la kuboresha utendaji, ambapo kwa sasa kuna andiko linalochakatwa likilenga kuibadili NEMC kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA). 

Alisema hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kisheria wa taasisi hiyo katika utekelezaji wa sera na sheria za mazingira.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuongeza uelewa wa kisheria juu ya usimamizi wa mazingira nchini. 

Alifafanua kuwa uelewa mdogo miongoni mwa wadau mara nyingi umekuwa ukisababisha migongano ya kisheria na kanuni kati ya taasisi mbalimbali.

Dk. Semesi aliongeza kuwa mafunzo hayo yanashirikisha mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na mawakili kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.