Ili kuzalisha fursa za ajira kwa vijana na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya, Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan ameahidi kuanzisha kongani za viwanda.
Mbali na hilo, Dk Samia amesema atakapochaguliwa kuwa Rais wa Tanzania kwa awamu nyingine, ataangalia uwezekano wa kujenga daraja katika eneo la Mwanjelwa kuwawezesha wananchi kuvuka barabara kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Dk Samia ameyasema hayo leo, Septemba 4, 2025 wakati wa mkutano wake wa kampeni katika Jimbo la Mbeya mjini, mkoani Mbeya.
Amesema kongani hizo ni kwa ajili ya sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo au madini, akilenga kuwaongezea vijana uwezo wa kushindana na kunufaika na shughuli za uzalishaji.
"Tunakwenda kuweka kongani za viwanda ili vijana wa Mbeya waongeze thamani mazao yao na wanayokwenda kuyauza sokoni, wapate faida zaidi," amesema Dk Samia.
Amesema kuelekea mwaka 2030, kuna ajenda ya kuifanya sekta ya kilimo ikue kwa asilimia 10 kutoka asilimia sita ya sasa, ndiyo maana hatua mbalimbali zinachukuiwa kufanikisha hilo.
Katika hatua nyingine, Dk. Samia ameahidi kuweka taa za barabarani katika maadhi ya maeneo ya Jiji la Mbeya ili kuwawezesha vijana kuendesha shughuli zao za kiuchumi hata wakati wa usiku.
"Ninawaahidi kwamba nikipata ridhaa nitaweka taa za barabarani pale Ilomba, Meta na njiapanda ya Uyole - Kyela ili vijana wetu wajiajiri na kufanya kazi wakati wote," amesema na kuibua shangwe kutoka kwa wananchi.
Pia, amesema Serikali itajumuisha huduma za uzazi katika kitita cha huduma muhimu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) utatumika kugharimia na wasio na uwezo ndiyo wataingia humo.
“Wale ambao hawana uwezo kabisa ndiyo wataingia kwenye kundi hili, lakini wale wenye uwezo, wanaozaa kwa raha na kujipangilia, hao watatuchangia,” amesema.
Katika maeneo yote aliyopita, Dkt Samia ametoa ahadi kwa wananchi zinazolenga kuchochea maendeleo na ustawi wao hasa katika huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi.
Mapema asubuhi akiwa mji wa Mbalizi, Dkt Samia ameahidi kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwani matokeo ya ruzuku hizo yamekuwa ni makubwa hususani kwa Mkoa wa Mbeya ambako wanazalisha zaidi mazao ya pareto, mahindi, mpunga na maparachichi na asilimia 85 ya wananchi wake ni wakulima.
Amewahakikishia kwamba uwezo wa Serikali kutoa ruzuku bado upo, hivyo amewataka wajisajili na kutunza namba za siri huku akionya kwamba mbolea za ruzuku siyo kwa ajili ya kuuzwa.
"Nakumbuka nilipokuja hapa mlinieleza kwamba hitaji lenu kubwa ni mbolea. Nililifanyia kazi, mbolea imegawiwa na wakulima wamenufaika. Lengo letu tuzalishe, tujilishe na ziada tuuze kama mazao ya biashara. Tanzania tuna ziada ya chakula, niwashukuru sana wakulima.
"Niwaombe sana wakulima, mkajisajili kupata ruzuku ya pembejeo kwani uwezo wetu wakutoa ruzuku upo. Mbolea tunazotoa kwa ruzuku siyo kwa ajili ya kuuzwa, msishirikiane na waovu kuuza vitu vinavyotolewa kwa ruzuku," amesema.
Kwa upande wa sekta ya mifugo, Dkt Samia ameahidi kukamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Utengule. Pia, ameahidi kwamba wanakwenda kuitambua mifugo yote iliyopo nchini na kuichanja ili kujihakikishia soko la nyama la nje ambalo linazingatia viwango vya ubora.
"Niwahakikishie ndugu zangu, huko nje kuna soko kubwa la nyama, lazima tujipange kutumia fursa hiyo," amesema.
Amesema watakuja na mfumo utakaohakikisha ndugu wa marehemu wanalipa gharama za matibabu kabla na baada ya mgonjwa kufariki.
“Lakini ni marufuku kuzuia miili ya waliotangulia mbele za haki kwa sababu ndugu zake hawajalipa,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED