Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani linamshikilia Ally Shabani (29), mganga wa tiba asili na mkazi wa Makazi Mapya, Mlandizi wilayani Kibaha, kwa tuhuma za mauaji ya Juma Nyambihira.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Muhudhwari Msuya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), alisema tukio hilo lilifichuka baada ya ndugu wa marehemu kutoa taarifa ya kupotea kwake tangu Agosti 17, ambapo taarifa hizo zilipokelewa na Kituo cha Polisi Mlandizi mnamo Agosti 29 mwaka huu.
Kamanda Msuya alieleza kuwa baada ya taarifa hizo, polisi walifungua jalada la uchunguzi na kuanza kufuatilia, ambapo walimkamata mtuhumiwa Shabani aliyekuwa akiishi na marehemu Juma, akimpatia matibabu ya asili kutokana na tatizo la uoni hafifu.
Amesema kuwa Septemba 3, wakati upelelezi ukiendelea, polisi walifika nyumbani alipokuwa akiishi mtuhumiwa pamoja na marehemu kwa ajili ya upekuzi, na kubaini uwepo wa tanuri la mkaa karibu na nyumba hiyo. Kando ya tanuri hilo, kulionekana dalili za shimo.
“Baada ya kufukuliwa, tulibaini ndani ya shimo hilo ulikuwa mwili wa marehemu Juma Nyambihira,” alisema ACP Msuya.
Aliongeza kuwa mwili wa marehemu unatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED