Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanasajili kampuni na majina ya biashara zao ili kuepuka uvunjaji wa sheria na usumbufu wa kibiashara unaoweza kujitokeza endapo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Hayo yamesemwa na Afisa Leseni wa BRELA, Fransice Filimbi, wakati wa Maonyesho ya 20 ya Kibiashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea mkoani hapa. Filimbi alieleza kuwa lengo kuu la BRELA kushiriki katika maonyesho hayo ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuhusu umuhimu wa kusajili biashara zao pamoja na kuwaelekeza namna ya kupata huduma hizo kwa njia ya mtandao.
“Wale wanaotembelea banda letu wanapatiwa msaada wa moja kwa moja wa usajili, na mara baada ya mchakato kukamilika, wanapokea vyeti vyao hapo hapo,” alisema Filimbi.
Kwa mujibu wa Filimbi, biashara iliyosajiliwa hupewa utambulisho wa kisheria unaomwezesha mfanyabiashara kufanya kazi kwa uhuru zaidi, kujiamini, na kupata fursa mbalimbali kama vile mikopo kutoka taasisi za kifedha na kushiriki katika zabuni mbalimbali za kibiashara.
Aidha, Bahati Athumani, mmoja wa wafanyabiashara waliotembelea banda la BRELA, aliipongeza taasisi hiyo kwa huduma wanazotoa na kuomba elimu ya usajili wa biashara isambazwe zaidi ili kuwafikia wafanyabiashara wengi walioko pembezoni.
“Wafanyabiashara wengi tumekuwa tukipoteza fursa muhimu kwa sababu ya kutojua umuhimu wa kusajili majina ya biashara, alama za bidhaa na hata ubunifu. Tunaiomba BRELA waendelee kutufikia kule tuliko ili kutupa elimu ya moja kwa moja,” alisema Bahati.
Aliongeza kuwa baada ya kusajili jina la kampuni yake katika banda hilo, amepata uelewa na kujiamini zaidi katika biashara yake. “Hili linatusaidia kuepuka migogoro ya kibiashara na kujenga biashara zetu kwa misingi imara ya kisheria,” alisisitiza.
Kwa ujumla, BRELA imejidhatiti kuhakikisha wafanyabiashara wote wanapata elimu na huduma stahiki za usajili, huku ikihimiza kila mmoja kutumia fursa zilizopo kabla ya hatua kali kuchukuliwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED