Biden afanyiwa upasuaji kudhibiti saratani ya ngozi

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:50 PM Sep 05 2025
Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden.
Picha:Mtandao
Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden.

RAIS wa zamani wa Marekani, Joe Biden, amefanyiwa upasuaji wa saratani ya ngozi hivi karibuni, msemaji wake ameeleza.

Msemaji huyo wa Biden ameiambia CBS News, ingawa hakutoa maelezo zaidi.

Upasuaji huo hutumika kukata ngozi hatua kwa hatua hadi pale ushahidi wa saratani unapokoma kuonekana.

Biden, mwenye umri wa miaka 82, ameonekana siku za karibuni akiwa na jeraha upande wa kulia wa kichwa chake.

Mwaka 2023, Biden aliondolewa kidonda cha saratani ya ngozi kifuani wakati wa uchunguzi wa kawaida wa kiafya.

Mwezi Mei, aligunduliwa kuwa na saratani ya tezi dume (prostate cancer), ambayo tayari imeenea hadi kwenye mifupa.

“Saratani inatugusa sote,” Biden aliandika kwenye mitandao ya kijamii wakati huo. “Kama wengi wenu, mimi na Jill tumegundua kuwa tunakuwa imara zaidi katika sehemu zilizojeruhiwa.”

Biden pia aliwahi kuondolewa aina kadhaa za saratani zisizo za melanoma hapo awali, kabla hajawa rais.

Tangu aondoke Ikulu Januari mwaka huu, amejitenga kwa kiasi kikubwa na macho ya umma na kufanya machache tu ya hadhara.

Familia ya Biden kwa muda mrefu imekuwa ikihimiza mapambano na tiba dhidi ya saratani. Mtoto wao mkubwa, Beau, alifariki mwaka 2015 kutokana na saratani ya ubongo.

Licha ya upasuaji wa ngozi wa hivi karibuni, mtandao wa Inside Edition, jana Septemba 04, ulichapisha video ya Biden, akitoka kanisani Rehoboth Beach, Delaware, akiwa na jeraha kwenye paji la uso.

BBC, PEOPLE