Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Kisabya, amewahakikishia Watanzania kuwa amani itabaki kuwa nguzo kuu ya taifa endapo atachaguliwa kuwa Rais.
Akihutubia wakazi wa Buzebazeba, Manispaa ya Kigoma Ujiji, leo, Kisabya amesema usalama wa raia na kudumu kwa amani ndicho kipaumbele kikuu cha chama chake.
“Usalama wa watu ni jambo la msingi kuliko kitu kingine chochote. Ni amani ndio inatufanya tuwe hapa. Wanasiasa wachezee kila kitu ila wasichezee amani yetu. Mchukue kila mnachotaka ila amani yetu mtuachie,” amesema Kisabya.
Katika sera zake, Kisabya ameahidi:
Aidha, Kisabya amesisitiza kuwa serikali yake itapambana vikali na vitendo vya ushoga na usagaji, akieleza kuwa “maovu hayo hayana nafasi katika jamii ya Tanzania.”
Kisabya amewataka vijana kuacha kususia uchaguzi na badala yake wajitokeze kupiga kura:
“Siasa ni chombo cha mabadiliko, na kila kura ina umuhimu mkubwa katika kuboresha maisha ya Watanzania. Vijana msipoteze nafasi hii,” amesisitiza.
Baada ya mkutano huo, Saida Ramadhani, mkazi wa Kigoma, amesema amefurahishwa na msimamo wa Kisabya kuhusu kulinda amani:
“Amani ndiyo nguzo ya maendeleo ya kila Mtanzania, sera zake zimetupa matumaini,” amesema.
Naye kijana Yusuph Omary amehimiza vijana kujitokeza kwenye mikutano na kusikiliza sera ili wafanye maamuzi sahihi siku ya kupiga kura.
Chama cha NRA kimekuwa cha kwanza kuzindua kampeni zake mkoani Kigoma na chama cha kumi kitaifa kuzindua kampeni tangu kuzinduliwa rasmi Agosti 28 mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED