Dk. Samia: Wakulima parachichi neema inakuja

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:39 PM Sep 05 2025
Dk. Samia: Wakulima parachichi neema inakuja

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwawekea miundombinu mizuri wakulima wa parachichi wilayani Rungwe mkoani Mbeya, ili kuwa imara wakati wote pindi soko litakashuka na kuimarika.

Dk. Samia ameyasema hayo leo  Ijumaa, Septemba 5, 2025 wakati akiwahutubia wananchi wa Mji wa Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya katika mkutano wa hadhara ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za kusaka kura za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

“Wajibu wetu hata kama soko zuri au baya, wajibu wetu kuwasaidia wakulima, ndicho tutakachoenda kukifanya. Kwenye parachichi tutajenga vituo 50 vya kuhifadhia zao hili, viwili vitakuwa hapa Rungwe.

“Vituo ambavyo vitakuwa na ubaridi wa kuhifadhia parachichi na mazao mengine ya mbogamboga ili kuvuta muda wakati mataifa mengine yamezalisha zao hili na kuuzwa duniani za Tanzania zitakuwa zinavuta muda,” amesema.

Dkt Samia ameongeza vituo vitakavyojengwa vitakuwa na uwezo wa kuhifadhi parapachichi kwa miezi mitatu ili soko la dunia lipande kisha wakulima kuuza.