Mgombea urais NLD ataja misingi sita ya kuiongoza Tanzania

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 04:51 PM Sep 05 2025
Mgombea wa urais kwa tiketi ya National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea wa urais kwa tiketi ya National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo.

Mgombea wa urais kwa tiketi ya National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amezindua kampeni yake ya kitaifa jijini Tanga na kutaja misingi sita itakayokuwa msingi wa uongozi wa chama hicho endapo kitapata ridhaa ya wananchi kuingia Ikulu.

Doyo amesema kwamba NLD haikubahatishi kuingia madarakani, bali imejipanga na mikakati madhubuti ya kuongoza taifa, huku dira yake ikiwa ni kujenga Tanzania yenye maendeleo jumuishi.

“Maendeleo jumuishi yenye uchumi imara unategemea uzalishaji wa ndani, haki, ustawi na usawa wa kila Mtanzania. Ili kufanikisha dira hii, NLD litaongozwa na misingi mikuu sita,” amesema Doyo.

Misingi hiyo sita ni:

  1. Uzalendo, haki na maendeleo pamoja na haki ya usawa kwa kila Mtanzania.
  2. Uwajibikaji na uongozi unaozingatia maadili ya kitaifa.
  3. Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kijamii.
  4. Kuhifadhi na kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
  5. Ujenzi wa taasisi imara zitakazowajibika kwa wananchi.
  6. Maendeleo yanayozingatia mazingira na matumizi endelevu ya teknolojia.

Aidha, Doyo ameahidi kwamba endapo atapata ridhaa ya wananchi, atahakikisha changamoto zote zitatatuliwa na uchumi unainuliwa ili wananchi wote, hasa walioko kwenye umasikini licha ya utajiri wa taifa, waweza kunufaika.

“Nchi yetu siyo masikini, lakini sisi tunaitwa wanyonge. Sasa ili msiitwe wanyonge, msifanye mchezo, changamkeni Oktoba 29, nendeni mnichague Doyo Hassan Doyo. Nitakwenda kubadilisha kila penye changamoto,” alisema Doyo.