Madeleka aahidi bima ya afya kwa kila mwanajimbo Kivule

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:57 PM Sep 05 2025

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kivule kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Wakili Peter Madeleka.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kivule kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Wakili Peter Madeleka.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kivule kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Wakili Peter Madeleka, amesema endapo atachaguliwa ataweka utaratibu wa kuhakikisha kila mwanajimbo anapata bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni zake, Madeleka amesema atatumia taaluma yake ya sheria kuleta mabadiliko ya kweli katika jimbo hilo, akisisitiza kuwa amechoshwa kuona fursa zikifunikwa na ubadhirifu wa viongozi waliokosa uwajibikaji.

Amebainisha kuwa jimbo la Kivule linakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu mibovu ya barabara, huku akidai hata barabara zilizopo hazijaunganisha kata zote sita kwa kiwango cha lami.

“Mzigo mzito huwa anapewa Mnyamwezi… tangu tupate uhuru Kivule bado ndilo eneo lenye barabara duni zaidi. CCM iliahidi kujenga barabara kwa kutumia zaidi ya Sh bilioni 213 katika jimbo la Ukonga, ambapo Kivule imo, lakini hadi leo hamjaona lami hapa?” alihoji Madeleka, na kushangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Ameongeza kuwa kuwapa CCM miaka mingine mitano ya uongozi ni sawa na kukubali kuendelea kuishi na kero ya barabara za vumbi na matope, hivyo aliwataka wananchi wamchague yeye pamoja na madiwani wa ACT-Wazalendo.

Kuhusu sekta ya afya, Madeleka amesema wapo wananchi wanaopoteza maisha kwa kukosa matibabu kutokana na uzembe wa serikali kushindwa kuweka vifaa tiba kwenye hospitali.

“Juzi mlikuwa mnasikia CCM wakisema wakichaguliwa tena wataacha kuzidai maiti. Sisi hatusubiri kuingia bungeni. Tayari tumeshachukua hatua – tulilipia gharama za kuzikwa kwa wananchi 17 ambao miili yao ilizuiliwa kwa siku 48 katika hospitali tofauti hapa Dar es Salaam. Hatuwezi kuwa na utawala wa kidhalimu unaodai hata maiti,” amesema.

Ameahidi pia kuhakikisha kila mjamzito anajifungua salama kwa kuboresha huduma katika kila kituo cha afya endapo atapewa ridhaa na wananchi.

Madeleka amerejea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akisema kila mwaka takribani Sh bilioni 48 zinaporwa na baadhi ya viongozi wa halmashauri, na kuwataka wananchi wasiwape tena nafasi viongozi hao kuomba ubunge.

Aidha, ameahidi kupigania vijana wapate mikopo ya kuendeleza biashara na ajira, akisema tatizo la ukosefu wa ajira ni zao la sera mbovu za CCM.

“Nikichaguliwa, ofisi yangu itakuwa wazi saa 24 kwa wananchi wangu wote ili kusikiliza na kutatua kero zao,” amesisitiza.