Mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha EATV, Marco Kilo amedaiwa kushambuliwa wakati akiendelea na majukumu yake ya kihabari katika kituo cha mabasi yaendayo kasi cha Mbezi Luis juzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN) ya jana, Edwim Soko, Marco alikamatwa katika kituo cha mabasi cha Mbezi Luis alipoenda kwa maofisa wa UDAT kupata mizania ya habari aliyokuwa akiifuatilia ya msongamano wa abiria katika kituo hicho kutokana na uchache wa mabasi.
“Kwa maelezo yake ameniambia kuwa baada ya kujitambulisha maofisa hao badala ya kumpa ushirikiano walianza kumshambulia kwa kipigo na kisha wakafika polisi na kumfunga pingu na kumpeleka Kituo cha Polisi cha Stand ya Magufuli”
“Hapo aliandikishwa maelezo na kuachiwa saa 2.00 za usiku huku simu yake ikishikiliwa hapo polisi, Mwandishi Marco aliambiwa arudi leo (jana) kwa jail ya kufikishwa Mahakamani, alipofika kituo cha polisi aliambiwa arudi nyumbani na kama akihitajika basi watampigia simu. Walimpa simu yake baada ya kufutwa kwa picha alizokuwa amezipiga kwenye kituo cha mabasi yaendayo kasi cha Mbezi Luis” imesema sehemu ya taarifa ya Soko.
Aidha kwa mujibu wa taarifa ya Soko, baada ya Mwandishi Marco kuambiwa arudi nyumbani aliomba RB ili akatibiwe lakini aliambiwa akamuone Mkuu wa Kituo baada ya kumuona akaambiwa akamuone mpelelezi wa kituo ,hata hivyo hatimaye alipewa RB yenye namba MGF/RB/6316/2025. Mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha EATV, Marco Kilo akiwa hospitali kutibiwa
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED