Wakati kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu zikiingia siku ya sita, baadhi ya wanachama wa chama hicho wamesema vipaumbele vinavyonadiwa na mgombea wa CCM vitaleta matokeo chanya kwa Watanzania.
Wakizungumza leo Septemba 3 wilayani Meatu, mkoani Simiyu, wanachama hao wamesema kampeni hizo zimethibitisha kazi zilizotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hususan miradi ya kimkakati ya miundombinu ambayo imeboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya taifa.
Kada wa CCM kutoka mkoani Mara, Mason Kimbo, amesema safari ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu imeendelea kwa mafanikio makubwa katika mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu, ikionesha mwitikio chanya wa wananchi kwa sera na Ilani ya chama hicho.
“Kampeni zilianza Mwanza, ambako tulimpokea na kumsikiliza Mgombea Mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi. Baadaye safari iliendelea Mara, wananchi walijitokeza kwa wingi na kuonesha ukarimu mkubwa, kisha kuelekea Simiyu ambako Dk. Nchimbi alipokelewa Itilima na Meatu,” amesema Kimbo.
Amebainisha kuwa wananchi wamekiri kazi za Rais Samia zinazoonekana kupitia miradi ya miundombinu ni ushahidi wa mabadiliko makubwa, na kwamba vipaumbele vya CCM kwa mwaka 2025–2030 vinadhihirisha dhamira ya kujenga Tanzania yenye sura mpya, vikilenga sekta za afya, viwanda na ajira.
“Katika siku za mwanzo baada ya Uchaguzi Mkuu, chama kimepanga kutoa ajira zaidi ya vijana 12,000. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vyetu vinavyogusa maisha ya kila Mtanzania,” amesema Kimbo, huku akitoa wito kwa wananchi kushiriki ipasavyo katika kupiga kura.
Kwa upande wake, kada wa CCM kutoka Itilima, Njalu Silanga, amesema Ilani ya chama hicho imelenga kumkomboa Mtanzania na kuleta maendeleo ya kitaifa kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati na yenye tija kwa wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED