Tanzania yawavutia wawekezaji Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:50 PM Sep 05 2025
Meneja Mtafiti kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Anna Lyimo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja Mtafiti kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Anna Lyimo.

Serikali ya Tanzania imekutana na wawekezaji katika Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AFSF2025) linaloendelea jijini Dakar, Senegal, kwa ajili ya kuwasilisha taswira mpya ya uwekezaji isiyo na vikwazo—hatua iliyowavutia wawekezaji na viongozi wa kimataifa.

Akizungumza kwenye Siku ya Uwekezaji Tanzania, Meneja Mtafiti kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Anna Lyimo, alisema serikali imeondoa urasimu na vizuizi vilivyokuwa vikikwamisha uwekezaji wa kimkakati.

“Kwa sasa Tanzania inatoa fursa za kipekee kupitia Kituo cha Huduma Pamoja (One Stop Centre), ambapo taratibu zote muhimu za uwekezaji hukamilika sehemu moja – kuanzia uhamiaji, kodi, leseni hadi masuala ya ajira,” alisema Lyimo.

Miongoni mwa vivutio vilivyotangazwa ni pamoja na:

  • Likizo ya kodi,
  • Uagizaji wa bidhaa bila ushuru,
  • Uhakika wa kuhamisha faida kwa asilimia 100,
  • Msamaha wa kodi wa hadi miaka 10 kwa wawekezaji watakaoingia katika maeneo maalum ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Wizara ya Kilimo, Dk. Stephen Nindi, aliwaeleza wawekezaji kuhusu miradi ya kilimo na kusisitiza juu ya mpango wa vijana Build a Better Tomorrow (BBT) unaotekelezwa na serikali, ambao tayari umeanza kuonyesha matokeo chanya.

Jukwaa la AFSF2025 limekusanya zaidi ya washiriki 6,000 wakiwemo marais, mawaziri, wawekezaji, wafanyabiashara wakubwa na mashirika ya kimataifa.

Ujumbe wa Tanzania katika jukwaa hilo ulihusisha Waziri Mkuu Mstaafu na Mshauri wa Rais, Mizengo Kayanza Peter Pinda; Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Kisaka Meena; pamoja na Dk. Stephen Nindi, Naibu Katibu wa Wizara ya Kilimo.

1