Mgombea wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema hakuna tatizo wala aibu kwa chama hicho kusafirisha wanachama wake kwa magari kwenda kuhudhuria mikutano ya kampeni.
Akihutubia leo Septemba 5, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Tukuyu, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, Samia alisema hatua hiyo inalenga kuwasaidia wanachama wanaoishi maeneo ya mbali ndani ya wilaya husika ili waweze kufika kwa urahisi kwenye viwanja vya mikutano.
“Nimesikia waandishi wa habari jana (juzi) wakimwambia Mwenezi kwamba CCM kinasafirisha watu kwa magari ndio maana mikutano inajaa. Lazima tutoe watu. Huwezi kutegemea mtu atoke umbali wa kilometa 90 au 100 kwa miguu hadi kufika hapa Uwanja wa Tandale. Ni lazima tuwasaidie usafiri. Lakini hatutoi watu kutoka wilaya moja kwenda nyingine, tunasafirisha waliomo ndani ya wilaya husika,” amesema Samia.
Amesisitiza kuwa kitendo hicho hakina tatizo kwa kuwa kinawasaidia wananchi wenye nia ya kusikiliza ilani ya CCM pamoja na utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na chama hicho.
“Siyo shida wala siyo aibu kwa chama kusafirisha wanachama wake kuja kusikiliza ilani ya chama inasemaje na yale tuliyoyatekeleza,” ameongeza.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Samia amewashukuru wananchi wa Tukuyu na Rungwe kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo wa kampeni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED