Mgombea urais CUF aahidi elimu bure hadi Chuo Kikuu

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:14 PM Sep 05 2025
Mgombea Urais wa CUF Gombo Samandito Gombo akinadi sera kwa wananchi wa Shinyanga.
Picha: Marco Maduhu
Mgombea Urais wa CUF Gombo Samandito Gombo akinadi sera kwa wananchi wa Shinyanga.

Mgombea wa urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, ameahidi kuwa endapo atashinda Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu, serikali yake itahakikisha elimu inatolewa bure kuanzia darasa la awali hadi chuo kikuu.

Akizungumza jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Stendi ya Mabasi ya Wilaya ya Shinyanga, Gombo alisema elimu ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya taifa, hivyo CUF ikipewa ridhaa ya kuongoza nchi itahakikisha kila mtoto Mtanzania anapata nafasi sawa ya kusoma bila kikwazo cha ada.

“Tukipewa ridhaa, kila mtoto atasoma bure kuanzia darasa la awali hadi chuo kikuu. Elimu ndiyo msingi wa maendeleo, na serikali ya CUF itawekeza kwa nguvu zote kwenye sekta hii,” alisema Gombo.

Mbali na sekta ya elimu, Gombo pia ameahidi kufuta gharama za matibabu ili wananchi wote wapate huduma za afya bure, sambamba na kufuta kikokotoo cha pensheni ambacho, kwa mujibu wake, kimekuwa kikwazo kwa wastaafu kunufaika ipasavyo na mafao yao.

“Kikokotoo kimekuwa mwiba kwa wastaafu kushindwa kunufaika na mafao yao. Serikali ya CUF itakifuta mara moja ili wastaafu wapate heshima ya stahiki zao,” aliongeza.

Aidha, aliahidi serikali yake itapitia upya mikataba yote yenye utata, ikiwamo ya bandari, kwa lengo la kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania.

Akizungumzia masuala ya kisiasa, Gombo pia aliahidi kufuta kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ili awe huru kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Katiba Mpya, akisema hatua hiyo ni hitaji la Watanzania kwa ajili ya mabadiliko ya kweli.

Kwa upande wake, mgombea mwenza, Husna Abdallah, alisema iwapo CUF itashinda urais, serikali yao itaubadilisha kiuchumi mkoa wa Shinyanga kutokana na utajiri mkubwa wa madini uliopo.

“Shinyanga ni mkoa wenye rasilimali nyingi hasa madini, lakini wananchi wake bado ni maskini. Tukishika dola, tutahakikisha rasilimali hizi zinawanufaisha wenyeji na kuondoa umaskini uliopo,” alisema Husna.

Alisisitiza kuwa maamuzi ya nani atawaletea maendeleo Watanzania yapo mikononi mwao siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 28 mwaka huu, na kuwataka kumchagua kiongozi sahihi kupitia CUF.