Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amewataka wataalamu 12 wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) walioko mafunzoni nchini humo kujituma na kujifunza kwa bidii, akisisitiza kuwa taifa linawategemea katika kuhakikisha usalama wa nishati ya umeme.
Watanzania hao walianza mafunzo ya kuendesha mitambo ya kufua umeme kwa gesi katika kampuni ya Siemens kuanzia Agosti 24 na yanatarajiwa kukamilika Septemba 13, 2025.
Balozi Matinyi alitoa wito huo jana wakati wa ziara yake nchini Sweden, ambapo pia alishawishi kampuni za Ericsson na Siemens Energy kuongeza uwekezaji na kuendeleza teknolojia zao nchini Tanzania.
Amesema mafanikio ya ziara hiyo ni kielelezo cha uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Sweden, hususan kupitia utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Katika ziara hiyo, Septemba 2 alitembelea kampuni ya Ericsson jijini Stockholm na kuzungumza na viongozi na wataalamu wake wakiongozwa na Mkurugenzi wa Sera za Serikali na Uhamasishaji, Ola Bergström.
Septemba 3, Balozi Matinyi alitembelea ofisi za Siemens Energy mjini FinspĂĄng na kupokelewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Gunnar Wik, pamoja na timu yake ya menejimenti na wataalamu.
Katika mazungumzo hayo, kampuni hizo ziliwasilisha mapinduzi ya kiteknolojia, yakiwemo matumizi ya mtandao wa intaneti wa kasi ya 5G unaoshirikiana na akili bandia (AI) kutoa huduma katika sekta mbalimbali.
Mhandisi wa kampuni hiyo, Jon Gamble, alisema teknolojia hiyo kwa sasa inatumika nchini Sweden kwenye huduma za magari ya wagonjwa, zimamoto, polisi, kilimo, elimu, afya, pamoja na usimamizi wa miundombinu ya reli, bandari, viwanja vya ndege, usafirishaji umeme na uchimbaji madini.
Ericsson imesema iko tayari kushirikiana na kampuni za simu Tanzania kusambaza teknolojia ya 5G nchini, ambako bado haijafika.
Kwa upande wake, Siemens Energy ilionesha teknolojia yake ya mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi, ikiwemo ile inayotumika katika kituo cha Ubungo, Dar es Salaam. Kampuni hiyo pia imedhamiria kuendelea kushirikiana na Tanzania kwenye miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme wa gesi katika maeneo ya Kinyerezi (Dar es Salaam), Mkuranga (Pwani), Somanga (Kilwa, Lindi), Dodoma na Mtwara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED