Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imemhukumu Erasto Moleli (35) adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya Josephina Dismas, huku mshtakiwa wa pili, Samwel Mchaki (49), akiachiwa huru kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja dhidi yake.
Hukumu hiyo ilisomwa Machi 10, 2025, na Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, ambaye alisema ushahidi wa kimazingira na sampuli zilizowasilishwa mahakamani zilionyesha bila shaka kuwa mshtakiwa wa kwanza, Erasto Moleli, alihusika moja kwa moja na mauaji ya Josephina, aliyekuwa akiishi naye kama mke na mume.
Jaji Kilimi alibainisha kuwa hata katika utetezi wake, Moleli hakukanusha shtaka hilo, na ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilithibitisha kuwa mwili wa marehemu Josephina ulitambuliwa kuwa wa mwanamke aliyekuwa akiishi na mshtakiwa huyo.
Kwa upande wa Samwel Mchaki, Jaji alisema hakuna ushahidi mwingine uliomtaja kama mshiriki wa mauaji hayo, isipokuwa tu kutajwa na mshtakiwa wa kwanza katika maelezo yake kwa polisi.
"Mshtakiwa wa pili aliunganishwa na kesi hii kutokana na kutajwa na mshtakiwa wa kwanza katika maelezo yake kwa polisi. Hata hivyo, hakuna sehemu nyingine ambapo ushahidi umeonyesha kuwa alihusika moja kwa moja katika tukio hilo. Kwa msingi huo, Mahakama inamuachia huru," alisema Jaji Kilimi.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mnamo Februari 19, 2023, majira ya alfajiri, washtakiwa walidaiwa kumuua Josephina Dismas na kisha kumchoma moto.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED