Aliyeukosa ubunge Kibaha Vijijini afunguka

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:23 PM Aug 29 2025
Aliyekuwa Mbunge jimbo Kibaha Vijijini Michael Mwakamo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Aliyekuwa Mbunge jimbo Kibaha Vijijini Michael Mwakamo.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Michael Mwakamo, amewatoa hofu wanachama wa chama hicho waliodhani kwamba atahama chama baada ya kukosa uteuzi wa kugombea nafasi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mlandizi, Mwakamo alisema kumekuwa na maneno mengi yanayosambaa baada ya kura za maoni, hali iliyosababisha sintofahamu miongoni mwa wanachama kuhusiana na msimamo wake kisiasa.

“Watu wengi wamekuwa wakipiga simu na wengine kufika nyumbani wakiwa na hofu kwamba ukimya wangu baada ya kura za maoni ni dalili ya kuhama chama. Siwezi kufanya hivyo, mimi ni mwana-CCM na nitaendelea kukipigania chama changu kishike dola,” amesema Mwakamo.

Ameomba wanachama na viongozi wa CCM katika Wilaya ya Kibaha Vijijini kuwa na mshikamano na kuacha maneno ya dhihaka dhidi ya walioshindwa kura za maoni.

“Wale waliokuwa wananiunga mkono nawaomba tuwe kitu kimoja kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo. Tusisikilize maneno ya watu, mimi niko vizuri na naendelea kushirikiana kutafuta kura,” ameongeza.

Aidha, Mwakamo ameishukuru Serikali kwa namna ilivyoidhinisha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi ambacho alikuwa mbunge wa jimbo hilo.