Aweso aingilia kati changamoto za vibarua Mradi wa Maji Kayanga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:05 PM Jul 25 2025
Aweso aingilia kati changamoto za vibarua Mradi wa Maji Kayanga

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ametoa maagizo kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa miji 28, Kayanga Wilayani Karagwe, kuhakikisha changamoto zinazowakabili vibarua wanaofanya kazi kwenye mradi huo zinatatuliwa.

Waziri Aweso amesisitiza kuwa ni lazima vibarua hao wapate mikataba ya kazi na maslahi yao yaweze kulipwa kwa wakati.

Katika ziara yake aliyoifanya kwenye mradi huo leo Julai 25, 2025, Waziri Aweso amekemea kitendo cha mkandarasi kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha haki za wafanyakazi zinaheshimiwa. 

“Kila anayefanya kazi anatakiwa kupewa ujira wake. Hawa vibarua wameshafanya kazi na kazi inaonekana hivyo, changamoto zao lazima zitatuliwe mara moja,” amesema Waziri Aweso.

Waziri Aweso pia ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 25.7, akisema kuwa mradi huo utaleta manufaa makubwa kwa jamii.

Aidha, Waziri Aweso amempongeza Mhandisi Magreth Nyange, msimamizi wa mradi huo, kwa utendaji kazi mzuri na kumteua kuwa Mkurugenzi wa mamlaka ya maji, ambapo amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri kumpangia kituo kipya cha kazi.