CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kinazindua kampeni Dar es Salaam, tayari kwa kunadi sera na ilani yake kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa mwaka 2025, huku kikiweka wazi ratiba kwa mikoa mingine nchini.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, huku mgombea wake wa urais, Samia Suluhu Hassan, na mgombea Mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, wakipeperusha bendera ya chama hicho.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini humo, alisema: “Baada ya uzinduzi huu, tutakwenda Mkoa wa Morogoro baadaye Dodoma. Kisha ratiba nyingine itapangwa. Kampeni ya mwaka huu zitakuwa za kiistoria na za aina yake.
“Tukio la kesho (leo) limebeba maono ya CCM. Tunazindua rasmi kampeni za chama chetu, tunakaribisha vyama vyote kuja kusikiliza sera zetu na Ilani ya Uchaguzi ya chama chetu iliyobeba matumaini, iliyobeba sekta zote na kutoa majawabu ya changamoto zilizoko ndani ya nchi,” alisema.
Kihongosi alisema chama kitaendelea kuheshimu Katiba ya nchi, utu na kuthamini vyombo vyote vya ulinzi na usalama na kulinda zao la amani kwa kuhakikisha wanafanya kampeni za kistaarabu.
“Mkoa wa Dar es Salaam wamepewa heshima kwa uzinduzi huu. Hakuna jambo dogo, kampeni zitaacha alama kwa nchi tangu kuanza kwa historia ya vyama vingi nchini,” alisema.
Kihongosi alisema katika uzinduzi huo, watawanadi na kuwaombea kura wagombea ubunge wanaogombea majimbo 12 ya mkoa wa Dar es Salaam pamoja na madiwani.
Alisisitiza kwamba kampeni za chama hicho zitakuwa za kistaarabu zikibeba misingi ya kulinda amani, utu na taifa.
“Tutakwenda kufanya kampeni kwa kutumia hoja, hakutakuwa na matusi, hatutatweza au kudhalilisha utu wa mtu mwingine. Chama kimejijenga katika misingi ambayo inatambua utu na kuamini binadamu wote ni sawa.
“Tutafanya kampeni ambazo zitakuwa na tija nzuri na Watanzania wataelewa kwa namna ambavyo wagombea wetu watakwenda kunadi sera zao na kuomba kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu,” alisema.
POLISI YAONYA
Jeshi la Polisi Nchini katika taarifa yake jana kuhusu kuanza kwa kampeni hizo limeonya wagombea na wafuasi wao pamoja na wananchi, kamwe asiwapo yeyote akawa chanzo cha kukiuka sheria, kanuni na taratibu wakati na baada ya kampeni hizo.
Kwa mujibu wa taarifa yake Msemaji wa Jeshi hilo, Naibu Kamishna (DCP) David Misime, Jeshi la Polisi limekumbusha kwamba jukumu la kudumisha amani, utulivu na usalama ni la kila mtu.
“Kamwe asiwapo mmoja wetu akawa chanzo cha kukiuka sheria, kanuni na taratibu wakati wote wa kampeni na baada ya kampeni, ili kuepuka vurugu au uhalifu wa aina yoyote ile kutokea.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kila mmoja kuzingatia ratiba na muda wa kampeni aliopangiwa ili kuepuka mivutano, migongano, migogoro au uhalifu kutokea, kwani hatutasita kumchukulia hatua kama sheria za nchi zinavyoelekeza,” alisema Misime katika taarifa hiyo.
CHALAMILA NA USALAMA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema ili uchaguzi uwe huru na wa haki, mikutano yote ya kampeni kwa mujibu wa taratibu inapaswa kufanyika vizuri na wao wana wajibu wa kuhakikisha amani na usalama unakuwapo wakati wote.
Alisema siku ya kupiga kura inatakiwa kusiwe na viashiria vyovyote vya vitisho vya ndani na nje ya nchi, ambapo viongozi wa serikali wana wajibu wa kulinda Watanzania katika mchakato huo.
“Lazima kuhakikisha mchakato wa upigaji kura unakuwa salama wa wazi na huru, ili mwishoni wathibitishe mchakato ulikuwa huru na haki,” alisema.
Chalamila alisema wamesikia katika mitandao namna wanavyoipa changamoto Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na pia mazingira mengineyo yanayoweza kuharibu taswira ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
“Watanzania hizi ndio nyakati za kuambiwa maneno mengi mno siasa chakula chake kikuu ni mitizamo,” alisema.
Alihamasisha Watanzania kuwafuatilia wagombea ili kumwona mwenye sera nzuri, ushawishi, mvuto, na kuchagua kunyoa au kusuka wakati wa upigaji kura.
Chalamila alivihakikishia vyama vyote vya siasa vitapata ulinzi wa kutosha ili kusiwe na mtu yeyote atakayeweza kumdhuru mgombea au chama chenyewe.
“Mtu yeyote atakayekuwa katikati ya kuharibu hiyo inayoitwa amani, wajibu wangu na vyombo vya dola tulionao ni kuthibiti hali hiyo, ili isikwamishwe mchakato wa uchaguzi,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED